Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vina mtaji mmoja ambao vinautegemea sana kuingiza kipato.

Mtaji huo ni hisia zako wewe unayefuatilia vyombo hivyo au kutembelea mitandao hiyo.

Moja ya hisia ambazo zinanufaisha sana vyombo hivi ni hofu. Vyombo hivi huwa vinachochea hofu ndani yako, inayokufanya uendelee kuvifuatilia ili ujue nini kinaendelea. Kwa hofu yako na kuendelea kuvifuatilia, vinapata hadhira ambayo wanaitumia kutangaza vitu zaidi na kupata fedha.

Hisia nyingine ambayo imekuwa inatumiwa sana na mitandao ya kijamii ni wivu. Hapa mitandao hii inakufanya ufuatilie maisha ya wengine, kuona nini kinaendelea. Na ili usiachwe nyuma, unahakikisha na wewe unaigiza maisha mazuri, kwa kupiga picha nzuri na kuziweka. Huku ukisahau kwamba unachofanya wewe ndiyo wanachofanya wengine pia, wivu wenu unawafanya muigize maisha, lakini anayenufaika ni mtandao wa kijamii mnaotumia.

Kuna hisia nyingine pia zimekuwa zinatumika, kama hasira, chuki, upendo na kadhalika.

Njia pekee ya kuepuka kutumika kama mtaji, ni kuepuka kabisa vyombo hivi na kama huwezi basi hakikisha hisia zako haziguswi. Usikubali hisia zako zichochewe na habari au tukio lolote lile. Jua mengi yanayotangazwa au kusambazwa kuibua hisia, yameongezwa chumvi kuliko uhalisia.

Na hata kwenye maisha yako ya kawaida, chanzo kikuu cha matatizo mengi unayokutana nayo kwenye maisha, huwa unayasababisha au kuyachochea wewe mwenyewe kwa kushindwa kudhibiti hisia zako. Hivyo zoezi hili la kudhibiti hisia lina manufaa makubwa sana kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha