Kushinda au kushindwa kwenye maisha ni matokeo ya msimamo wa kile ambacho mtu anafanya kwenye maisha yako.

Mfano kama mtu anafanya mazoezi kila siku bila kuacha, lazima atakuwa na afya bora.

Kama mtu anaweka akiba kwenye kila kipato bila kuacha, na kisha kuwekeza aiba hiyo bila kuitumia, lazima atafikia utajiri na uhuru wa kifedha kwenye maisha yake.

Kwenye kushindwa pia ni msimamo, tumia zaidi ya kipato chako kila wakati na kopa ili kutumia zaidi na utakuwa kwenye njia ya uhakika ya kwenda kwenye umasikini.

Sasa najua vizuri kwamba unajua msimamo ni muhimu.

Swala ni kwamba, siyo mara zote unaweza kuwa na msimamo kwa asilimia 100, maisha yana mambo yake, kuna wakati utakwama na kushindwa kufanya ulivyopanga. Lakini pia kuna wakati utakosea.

Wengi huwa wanaruhusu hali hizi za maisha au makosa wanayofanya yawe ndiyo mwisho wa safari yao ya mafanikio.

Unachopaswa kujua ni kwamba kosa moja halikuzuii kufanikiwa, kushindwa mara moja kufanya kile ulichopanga siyo mwisho wa safari yako.

Ila unapoendelea na makosa hayo au kuendelea kushindwa, tabia inajengeka na hiyo ndiyo inayokuangusha.

Kosa moja haliwezi kukuangusa, bali pale makosa hayo yanapojirudia ndiyo yanakupeleka kwenye anguko.

Kushindwa kuweka akiba mara moja hakuwezi kukuzuia kufikia uhuru wa kifedha, ila pale hiyo inapogeuka kuwa tabia, ndiyo tatizo linakuwa kubwa.

Kukosea mara moja ni ajali, kukosea mara mbili ndipo tabia inaanza kujengeka.

Hivyo wajibu wako wa kwanza kwenye maisha yako ya mafanikio ni huu; rekebisha makosa yako kabla hayajawa tabia.

Maana tabia ikishajengeka, ni ngumu sana kuivunja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha