Kama mtu hafanyi kazi yake vizuri, inaweza kuwa ni kwa sababu ya moja kati ya haya mawili.
Moja hajui jinsi ya kufanya kazi hiyo. Hivyo hapa tatizo ni ujuzi. Na ujuzi unaweza kutatuliwa kwa kumpatia mtu maarifa na mwongozo sahihi.
Mbili hawezi kufanya kazi hiyo. Hivyo hapa tatizo ni uwezo. Uwezo ni namna mtu alivyozaliwa, hivyo huna njia ya kubadili uwezo wa mtu kwenye eneo fulani.
Unaposhirikiana na watu, iwe ni umewaajiri au mmeingia ubia kwenye biashara au jambo lolote na kila ambacho mtu anapaswa kufanya hakifanyi kama anavyotegemewa, ni muhimu sana kujua tatizo lake ni ujuzi au uwezo.
Kama tatizo ni ujuzi unajua kazi ni rahisi, kumsaidia ajenge ujuzi anaohitaji ili aweze kufanya kazi yake vizuri.
Lakini kama tatizo ni uwezo, huna cha kufanya kubadili uwezo wake, bali unaweza kujua uwezo wake uko wapi na kisha kumpa majukumu yanayoendana na uwezo wake.
Watu huwa wanavurugwa pale wanapojaribu kutatua tatizo la uwezo kwa kutoa ujuzi zaidi, wanashangaa pamoja na kumjengea mtu ujuzi bado hafanyi anavyotegemewa na inakuwa rahisi kukata tamaa.
Lakini ukilijua tatizo sahihi na kulitatua, unapata majibu mazuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,