Kuna rafiki mmoja ambaye ni msikivu na aliye tayari kukusaidia muda wowote.

Rafiki huyu hahangaiki kukulazimisha ufanye chochote, bali atakuwa tayari kukusaidia pale unapoenda kwake kupata ushauri.

Rafiki huyu hahangaiki kukubadilisha, bali anakuambia kile kilicho sahihi halafu wewe unapaswa kufanya maamuzi yako sahihi.

Rafiki huyu ana hekima isiyo na ukomo, na huwa anaitoa taratibu na kwa unyenyekevu mkubwa. Ni wewe tu kuamua unaipokea na kuitumiaje hekima hiyo.

Rafiki huyu hataki chochote kutoka kwako, ila yupo kwa ajili yako muda wote, hata ule muda ambao haupo naye.

Rafiki huyo ni vitabu.

Hebu fikiria tena kuhusu vitabu, hakuna chochote unachotaka kujua sasa ambacho hakipo kwenye vitabu.

Na vitabu hivyo vimejaa hekima kubwa sana, lakini vimetulia, havikupigii kelele yoyote ile.

Ukichukua kitabu na kukisoma utapata hekima hizo, usipokisoma hekima hiyo haihami kwenda popote, na wala hakitalazimisha hekima hiyo ije kwako kwa sababu unaihitaji sana.

Mchague rafiki huyu, chagua vitabu ambavyo vitakuwa mwongozo wa maisha yako, vitabu ambavyo utakuwa unavisoma na kuvirudia mara kwa mara ili kupata hekima sahihi ya kuyaongoza maisha yako.

Popote unapokuwa, hakikisha rafiki huyu yupo karibu na wewe, muda wowote unaopata ambapo huna cha kufanya, badala ya kuupoteza kufuatilia mambo yasiyo na manufaa kwako, utumie kuzungumza na rafiki yako huyo ili akupe hekima iliyopo ndani yake.

Kwa dunia tunayoishi sasa na urahisi wa kupatikana kwa maarifa, huna sababu ya kujitetea kwa nini hujui kile unachopaswa kujua, kwa nini huna hekima na kwa nini hufanyi kwa ubora kile unachofanya. Ni uzembe tu unaoweza kuwa sababu ya wewe kukosa hekima, kwa sababu hekima zipo kwenye vitabu vingi unavyoweza kuvipata na kuvisoma, lakini hufanyi hivyo.

Usikubali kuendelea na uzembe, weka azimio sasa, chagua marafiki wako wa kweli na ambatana nao kila wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha