Kumekuwa na watu ambao wanaanzia chini kabisa, wanakuwa kiu kubwa ya mafanikio, wanajituma na kujisukuma mno. Jitihada zao zinawafikisha kwenye mafanikio makubwa.

Lakini baada ya mafanikio hayo, wanapotea kabisa. Wengi wanaanguka baada ya mafanikio yao ya awali, iwe ni kwenye biashara, kazi, michezo na hata fedha.

Moja ya vitu vinavyosababisha anguko hili baada ya mafanikio ni kusherekea ushindi kwa muda mrefu. Baada ya kupata ushindi ambao mtu alikuwa anautaka, anatumia muda mwingi kusherekea ushindi huo. Anaona ameshamaliza kila kitu na hakuna tena kinachoweza kumshinda.

Lakini maisha hayapo hivyo, asili haiendi hivyo. Kwenye asili, kila unapopata ushindi, kuna changamoto mpya zinaibuka mbele yako, ambazo ni kubwa kuliko zile ulizoshinda huko nyuma.

Hivyo kama unataka kubaki kwenye kilele cha ushindi, huna muda wa kupumzika na kusherekea, unahitaji kuendelea na juhudi za ushindi.

Ukishafanya kazi moja bora, unachopaswa ni kufanya kazi nyingine bora zaidi ya hiyo.

Ukianzisha biashara moja kwa mafanikio, ikuze zaidi biashara hiyo au anzisha biashara nyingine.

Ukiandika kitabu ambacho ni bora kabisa, unapaswa kuandika kitabu kingine bora kuliko hicho.

Ukipata fedha nyingi ulizokuwa unataka kupata, kinachofuata ni kuziwekeza vizuri fedha hizo ili ziweze kuzaa fedha zaidi.

Usitumie muda wako mwingi kusherekea ushindi wako wa nyuma na wala usifikiri ndiyo umemaliza kila kitu. Badala yake angalia ni changamoto ipi mpya iliyopo mbele yako na anza kuifanyia kazi mara moja.

Mafanikio ya kudumu kwenye maisha ni pale unaporudia rudia kufanya kilicho bora, kupumzika na kuona umeshamaliza ndiyo mwanzo wa anguko, epuka sana hilo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha