Kwenye uchumi, ukitaka kitu kipande bei, kiondoe sokoni, upatikanaji wa kitu unapokuwa mdogo, ghafla uhitaji wake unakuwa mkubwa na bei yake inakuwa kubwa pia.
Kwenye saikolojia ukitaka watu wapende au kufanya kitu, wakataze wasiwe nacho au wasikifanye. Mwambie mtoto asishike moto na hapo utakuwa umempa kitu cha kufanyia kazi, kuhakikisha anashika moto.
Hivyo ndivyo binadamu tulivyo, wakati kitu kipo kwa wingi tunakichukulia poa, tukiona kinapungua au kuondoka ndiyo tunakithamini.
Tafiti zimekuwa zinaonesha kwamba wakati wa vita au majanga yanayoua wengi, idadi ya watu wanaojiua huwa ni ndogo sana. Maisha yanakuwa na thamani sana pale unapokuwa una hatari kubwa ya kuyapoteza, hivyo unayalinda. Ila unapokuwa huna hatari ya kuyapoteza maisha, yanakuchosha na watu wanaamua kuyapoteza wenyewe, kwa kujiua.
Kuna watu ambao wameishi miaka mingi wakijiambia kesho nitafanya kitu fulani (labda kuandika kitabu) lakini miaka inaenda na hawafanyi. Siku moja wanakutana na hatari, labda wanaambiwa wana saratani, ambayo itawaua ndani ya miezi sita, ghafla wanapata nguvu ya kuanza kuandika na ndani ya muda mfupi wanakuwa wamekamilisha kitabu.
Ukiwa na siku 30 za kuandika ripoti, siku 10 za kwanza hutafanya chochote, siku 10 nyingine zinazofuatia utakuwa unajipanga, siku 10 za mwisho, utatumia siku tano kupata kila unachotaka, siku tatu kupangilia na siku 2 kuandika na kukamilisha ripoti, bila ya kulala kabisa.
Yote haya yanatufundisha kitu kimoja, hakuna asiyethamini alichonacho, ila kuna ambao wana upatikanaji kwa wingi wa kile walichonacho na hivyo wanachukulia pia. Ni mpaka pale wanapokuwa kwenye hatari ya kupoteza walichonacho, ndiyo watu wanathamini na kujali sana.
Kwa kuwa akili zetu zinafanya kazi pale kunapokuwa na uhaba, ni muhimu ujiweke kwenye mazingira yanayolazimisha uhaba kwako kama unataka kufanya makubwa.
Zipo njia mbalimbali, kama kujiwekea tarehe ya ukomo ambayo ni ya muda mfupi, kuweka makubaliano na mtu mwingine ambayo yatakulazimisha kufanya kwa haraka la sivyo itakugharimu sana. Kwa vyovyote vile, fanya uhaba kuwa halisi kwako na utapata msukumo mkubwa sana ndani yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,