Kwenye biashara ya huduma, ambapo unafanya kitu cha kipekee kwa wateja wako na kuwataka wakulipe kiasi kizuri cha wewe kuweza kufanya hivyo, hawakosekani watakaotaka wakulipe kiasi kidogo kuliko unavyotaka wakulipe.
Na sababu pekee watakayoitumia ni kwamba kuna wenzako ambao wanauza huduma kama zako kwa bei rahisi kuliko wewe.
Sasa unaposikia hilo, unaona kama wenzako wanakupita kwa kupata wateja zaidi, hivyo unakimbilia kushusha bei ili upate wateja zaidi.
Sasa unaposhusha bei, unakaribisha vitu viwili;
Cha kwanza ni unapunguza kipato chako, kitu ambacho kinakulazimu ufanye mambo mengine ili kipato chako kiwe vizuri, hiyo itapelekea wewe kupunguza ubora wa kazi unayofanya, na hapo kupoteza wateja wazuri.
Cha pili ni unawavutia wateja wasio sahihi, wateja wanaoangalia bei rahisi tu na siyo kuthamini kile unachofanya. Wateja hawa huwa wanakuwa wasumbufu sana, hivyo unajikuta unatumia muda mwingi kuhangaika na wateja hao, badala ya kuweka thamani zaidi kwenye huduma unayotoa.
Swali ni je utamjibuje mteja anayekuambia wenzako wanatoza bei rahisi kuliko wewe?
Jibu fuatilia mfano huu wa maongezi.
Mteja; Kocha, wenzako wanatoa huduma za ukocha kwa bei rahisi kuliko wewe.
Kocha; Vizuri, inaonekana kwao utapata unafuu zaidi, nashauri ufanye nao kazi.
Mteja; Lakini napenda kufanya kazi na wewe, maana unatoa thamani kubwa zaidi.
Kocha; Hiyo ndiyo sababu kwa nini gharama za wengine ziko chini na zangu ziko juu, thamani inatofautiana, hivyo kama unathamini ninachofanya, kuwa tayari kulipa zaidi.
Kitu kimoja unachopaswa kusimamia ni thamani kubwa unayoitoa, ambayo hakuna mwingine anayeweza kuitoa. Ukishaweza hilo, unakuwa huru kutoza bei kubwa kuliko wengine, na wateja (sahihi) hawawezi kukataa au kukulinganisha na hao wengine kwa sababu wanajua kwako wanapata thamani ambayo hawawezi kuipata kwa wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,