Kisayansi (fizikia) kazi inakuwa imefanyika pale nguvu inapokuwa imewekwa kwenye kitu, na kitu hicho kikasogea.

Hivyo kama nguvu imewekwa mahali lakini kitu hakijasogea, hakuna kazi iliyofanyika, hata kama nguvu iliyotumika ni kubwa kiasi gani.

Mfano kusukuma ukuta, haijalishi umesukuma kwa nguvu kiasi gani, hata kama umetokwa na jasho jingi, kama ukuta huo haujasogea au kuanguka, hakuna kazi iliyofanyika, nguvu hizo zimepotea bure.

Sasa turudi na hili kwenye maisha yetu ya kila siku.

Kuna juhudi nyingi ambazo unaweka, nguvu kubwa sana, lakini hazikuwezeshi kupiga hatua yoyote kwenye maisha yako. Hizi ni nguvu ambazo unakuwa umechagua kuzipoteza. Mfano kufuatilia habari mbalimbali, hasa zilizo hasi au za udaku, kufuatilia maisha ya wengine, kuzurura mitandaoni ili kuona wengine wanafanya nini. Unatumia nguvu nyingi, lakini matokeo yake hayakubadilishi au kukunufaisha kwa namna yoyote ile.

Kwa upande wa fikra pia kuna nguvu nyingi tunazopoteza. Fikra zozote hasi unazoziruhusu kwenye akili yako, ni kupoteza nguvu ya akili yako. Kwa sababu fikra hizo hasi hazikuwezeshi kupiga hatua yoyote, zinakujaza hofu na kukuzuia usipige hatua. Kibaya zaidi, fikra hasi zinatumia nguvu mara mbili ya fikra chanya, ndiyo maana unapokuwa na fikra zozote hasi, unachoka kuliko kawaida.

Ondoa fikra zozote hasi kwenye akili yako, haijalishi umekutana na mambo mabaya na magumu kiasi gani kwenye maisha yako, tafuta upande chanya. Kila jambo lina upande chanya kama utautafuta na huo utakunufaisha zaidi.

Kabla hujatumia nguvu zako, jiulize je zinakwenda kuzalisha kazi au zinakwenda kupotea. Mara zote jua ni matokeo gani unayotaka kupata kisha kabla hujafanya chochote, jiulize kinachangiaje wewe kupata kile unachotaka. Kama haika mchango usifanye, nguvu zako na muda wako ni rasilimali zenye uhaba, zitumie kwa umakini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha