Najua hakuna mtu mwenye akili timamu ambaye anaweza kukaa chini na kupanga kushindwa. Yaani kwa makusudi kabisa unapanga uingie kwenye biashara na upate hasara. Hilo huwa halitokei.

Lakini kila siku watu wanashindwa, kila siku watu wanaingia kwenye biashara na kupata hasara. Je hili huwa linatokeaje? Ina maana kushindwa ni ajali?

Majibu ni hapana, kushindwa siyo ajali, bali ni matokeo ya kitu kilichopangwa.

Unapanga kushindwa, pale unaposhindwa kupanga. Sijui umeelewa vizuri hapo. Yaani ukishindwa kupanga, basi maana yake umepanga kushindwa.

Unaingia kwenye biashara kwa sababu umeambiwa inalipa kweli, umeona wengine nao wanafanya, na wewe unaingia kichwa kichwa, huna mipango yoyote ya kujitofautisha kwenye biashara hiyo na kuwafikia wateja wengi zaidi. Unaingia kufanya biashara, unashindwa, halafu unajiambia hukuwa na bahati! Ulishindwa kupanga, na hivyo ukawa umepanga kushindwa, hivyo lilikuwa ni swala la muda tu.

Kwa kila kitu unachofanya, kuwa na mpango kamili, usifanye chochote kwa kubahatisha. Kaa chini na weka mpango, kisha fuata mpango huo, huku ukiuboresha zaidi kadiri unavyoendelea kujifunza kwa hatua unazochukua.

Ni vizuri kuwa na matumaini na mtazamo chanya kwamba mambo yanawezekana, lakini matumaini na fikra chanya siyo mkakati, unahitaji kuwa na mkakati sahihi utakaokuwezesha kushinda. Na kukosa mkakati huo, ni kupanga kushindwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha