“Use good thoughts of wise people; if you cannot create similar kind and wise thoughts, then at least do not distribute the false thoughts expressed by you and by others.” – Leo Tolstoy
Kama huwezi kupata mawazo mazuri wewe mwenyewe, basi tumia mawazo ya wenye hekima.
Ni mengi na ni bure kabisa kwako kuyatumia.
Usiwe mtu wa kusambaza mawazo ya uongo ambayo umetengeneza wewe au wengine, utasababisha madhara makubwa.
Sisi binadamu huwa tunapenda sana maelezo ya kila kitu.
Huwa haturidhiki na kitu mpaka tuweze kukielezea.
Hivyo kama maelezo hayapatikani, basi huwa tuna tabia ya kutengeneza maelezo yetu wenyewe, yanavyoendana na tunavyotaka sisi.
Mara nyingi maelezo hayo huwa siyo sahihi, lakini tunayasambaza kwa wengi, na hapo tunafanya uharibifu mkubwa zaidi.
Chukulia mfano umemsalimia mtu halafu hakuitika, hilo litakusumbua na haraka sana utaanza kutafuta maelezo ya kwa nini mtu huyo hajaitika.
Kama ukitumia mawazo ya wenye hekima, utapata maelezo labda hajasikia au ana mambo mengi yanamsumbua na kadhalika.
Lakini kwa kufuata mawazo yako mwenyewe utapata maelezo kwamba, amekununia, anafanya kusudi, anakuonea wivu kwenye mambo fulani na kadhalika.
Unaona wazi hapo jinsi mawazo yako mwenyewe yalivyo hatarishi,
Lakini mawazo ya wenye hekima ni bora na yanajenga vizuri.
Hivyo pale tunapotaka kupata maelezo ya kitu au kukielewa kwa undani, tutumie fikra zetu kama tunaweza kupata ukweli na kama hatuwezi basi tutumie mawazo ya wenye hekima.
Kamwe usitengeneze sababu zako za uongo na kuanza kuzisambaza kwa wengine.
Utafanya uharibifu zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania