“…the true secret of happiness lies in the taking a genuine interest in all the details of daily life…” — William Morris
Siri kuu ya furaha ni kuweka umakini kwenye kila eneo la maisha yako ya kila siku.
Chochote kile unachochagus kukifanya, weka mawazo yako yote kwenye kitu hicho.
Usifanye kitu chochote kwa kupita, bali fanya kama ndiyo kitu kikuu kwenye maisha yetu.
Unakosa furaha kwa sababu unachukulia poa sana vitu unavyofanya.
Unafanya ili tu kukamilisha na hivyo huweki umakini wako wote.
Unafanya haraka haraka halafu ukimaliza unakimbilia kwenye mitandao ya kijamii au kufuatilia habari au maisha ya wengine.
Sasa hapo umefaidika nini?
Ulichokuwa unakifanya hujakifanya vizuri, hivyo hujisikii vizuri na kufurahia ulichofanya.
Ulikokimbilia nako hakuna cha maana, unaishia kujiona mtupu na hata kukata tamaa.
Kama unataka kuwa na maisha bora, maisha tulivu na yenye furaha,
Basi weka umakini mkubwa kwenye chochote unachojiruhusu kufanya.
Unakula, basi mawazo yako yote yaende kwenye kula.
Unafanya kazi, basi umakini wako wote uwe kwenye kazi.
Na katika muda wa kupumzika, usiruhusu mawazo yako yahangaike na kitu kingine chochote.
Tatizo la wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kwa namna ambayo hawafanyi kazi wala hawapumziki.
Akiwa kwenye kazi anawaza mapumziko.
Akiwa kwenye mapumziko anawaza kazi.
Ondoka kwenye mtego huu, kwa kuchagua kufanya mambo machache na kuyapa umakini wako wote.
Usichukulie chochote poa, kama siyo muhimu kwako usifanye, na kama ni muhimu basi fanya kwa umakini mkubwa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania