Tunajua hili kuhusu furaha, kwamba kadiri unavyoikimbiza, ndivyo unavyoikosa. Lakini ukiishi maisha yako na kuiacha furaha itokee, inakuwa na wewe kila wakati. Furaha ni kama kipepeo, ukikikimbiza kinakimbia, ukitulia eneo sahihi kinakufuata.

Mafanikio pia ndivyo yalivyo, ukiyakimbiza huyakamati, kila wakati utajiona hufikii mafanikio unayoyataka. Lakini ukiacha kuyakimbiza, yanajitokeza yenyewe. Mafanikio ni matokeo ya kile ambacho unakifanya kwa msimamo.

Kama unataka kuandika kitabu na kila siku unakazana kufikiria kuwa na kitabu kilichokamilika, hutaweza kuwa na kitabu. Lakini ukaacha kuangalia kitabu kilichokamilika na badala yake kujiambia unaandika maneno elfu moja tu kila siku, ndani ya miezi miwili, utakuwa umeandika maneno elfu 60 ambayo ni ukubwa wa kitabu cha kurasa 250 mpaka 300.

Ukisikia maneno elfu 60 unaona ni mengi mno na huwezi kuyafikia, lakini ukiacha kuyaangalia hayo na kuangalia maneno elfu moja tu kila siku, utashangaa umeyafikia hayo maneno elfu 60 bila ya shida yoyote.

Kadhalika kwenye utajiri, unapojiambia unataka kufikia ubilionea unaweza kukata tamaa kwa kuziangalia tu hizo sifuri zilizopo kwenye bilioni. Lakini ukichagua mfumo wa maisha ambao utaufuata kila siku, kama kuhakikisha matumizi yako ni madogo kuliko kipato, huku ukiweka akiba na akiba hiyo kuiwekeza sehemu inayozalisha, unafikia utajiri mkubwa, ni swala la muda tu.

Kitu cha kujifunza na kuondoka nacho hapa ni kimoja, mchakato. Jua kule unakotaka kufika, jua mchakato sahihi wa kukufikisha, kisha usiangalie sana kule unakokwenda, bali angalia kutekeleza mchakato wa kila siku. Endelea kuboresha mchakato huo kadiri unavyokwenda na matokeo unayoyapata.

Usisumbuke sana na matokeo ya mwisho, wewe fuata mchakato sahihi na jipe muda na matokeo yataonekana yenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha