Ni mapacha unaopaswa kuwa nao kama unataka kufanikiwa kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako.

Hii ni kwa sababu mafanikio siyo rahisi, yanahitaji kazi sana na pia hayaji haraka, yanahitaji muda mrefu kujijenga.

Hii ni kanuni ya asili, ambayo inafanya kazi mara zote, na ukitaka kuthibitisha hilo, angalia wanyama na mimea. Kila kiumbe kina muda wake kufika kinakopaswa kufika, na katika njia yake, kuna magumu mengi ambayo kinapaswa kuvuka.

Hivyo jikumbushe hili kila wakati, kuwa mvumilivu na kung’ang’ana mpaka utakapopata unachotaka.

Utajaribu mara nyingi na kushindwa, lakini usikate tamaa, badala yake endelea kujaribu tena na tena. Haijalishi umeshindwa mara ngapi, kama hutakata tamaa, kama utaendelea kujaribu, kuna nafasi ya ushindi mbele yako.

Tumia uvumilivu na ung’ang’anizi kwenye hatua hizi tatu muhimu za mafanikio.

Kwanza jiulize ni kitu gani kinachokusumbua, kitu gani hukubali jinsi kilivyo. Iwe ni kwenye maisha yako, kazi yako au biashara yako. Labda kuna huduma fulani umekuwa unatafuta huipati, labda kuna namna ungependa vitu viwe lakini havipo hivyo. Hatua ya kwanza ni kujua kipi hasa kinachokusumbua.

Pili jua ni njia ipo bora ya kufanya kile kinachokusumbua. Hapa unajiuliza ni kwa namna gani unaweza kurekebisha kile kinachokusumbua, kupata kile unachotaka au kufanya mambo yawe kama unavyotaka wewe. Kwenye hatua hii ya pili unajua kilicho sahihi kufanya na kuweka mpango wa kukifanya.

Tatu ni kufanya kile kilicho sahihi ili kuondokana na kinachokusumbua. Na katika kufanya huku, hakikisha unafurahia ufanyaji huo. Na kuwa mvumilivu na mng’ang’anaji mpaka upate kile unachotaka. Kwa kuwa unachofanya ni sahihi, usikate tamaa pale unapokutana na magumu au kushindwa, vumilia na ng’ang’ana kwa kuweka juhudi na kujipa muda, utapata chochote unachotaka.

Kwa kukamilisha hatua hizi tatu, unaweza kurudia kwenye kitu kingine chochote. Kila siku unakuwa unafanyia kazi kile kilicho sahihi na kitakachokuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Kwa kumalizia kumbuka kwamba kwa chochote unachopitia, kuna mtu mwingine anapitia magumu kuliko wewe. Ni rahisi sana kujidanganya kwamba tunapitia magumu kuliko wengine, lakini ukiangalia kwa ukaribu, utagundua kuna wengine wanapitia magumu kuliko wewe, lakini hawajakata tamaa. Hivyo ni mwiko kwako kukata tamaa.

Vumilia na ng’ang’ana, na hakuna kitakachoweza kukuzuia usifanikiwe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha