Kwenye mchezo wowote ule, jukumu la kwanza la mchezaji ni kuwa ulingoni, kuwa uwanjani, mengine baada ya hapo ni juhudi.

Ni bora kuwa ulingoni na kupigwa, kuliko kuwa nje ya ulingo kabisa.

Timu ambayo ipo kwenye ligi kuu, hata kama inafungwa na kila timu, ipo kwenye nafasi nzuri kuliko timu ambayo iko nje ya ligi kabisa.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio, jukumu lako la kwanza ni kuwa kwenye ulingo, kuwa kwenye njia inayokufikisha kwenye kile ambacho unataka.

Iwe unafanikiwa kwenye njia hiyo au la, hilo ni swala jingine, lakini kwanza, hakikisha uko ulingoni.

Kadhalika kwenye mipango unayojiwekea, ukishajua nini unachotaka, mara moja nenda kwenye hatua za kukufikisha kwenye kitu hicho.

Acha kupoteza muda kwenye kufanya upembuzi na michanganuo, yote hayo ni nje ya ulingo.

Ingia ulingoni na hata kama utaambulia makonde, utajifunza njia bora ya kushinda.

Ukiwa nje ya ulingo mambo ni rahisi, angalia mashabiki wanavyokuwa rahisi kulaumu wachezaji waliopo ulingoni kwa kufanya makosa.

Ila ukiingia ulingoni, utaona ugumu wake na utajifunza mengi kuliko ukiwa nje ya ulingo.

Je upo ulingoni? Unachofanya sasa kina uhusiano wowote na kile unachotaka kupata au kufikia kwenye maisha yako?

Kama jibu ni hapana basi jua unajichelewesha, ni wakati wako sasa wa kuingia ulingoni. Ingia hata kama utaambulia makonde, ni bora kuliko kuwa nje ya ulingo kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha