Ukitaka kuwa na maisha tulivu, usiseme kila unachojua na usihukumu kila unachoona.
Ni asili yetu binadamu kusema kila tunachojua na hili limekuwa linatuingiza kwenye matatizo makubwa. Hasa pale unaposema kwa wale ambao hawapo tayari kupokea kile ambacho umewaambia, au wale ambao hawawezi kuking’amua. Hivyo kabla hujasema kila unachojua, jiulize kama wale unaowaambia wanaweza kukipokea na kukielewa. Kuna wakati unapaswa kukaa kimya hata kama unajua cha kusema, kwa sababu kusema kwako kutafanya mambo yawe magumu zaidi.
Pia ni asili yetu sisi binadamu kuhukumu kila tunachoona. Huwa hatuoni nguo, bali tunaona nguo nzuri au mbaya, kila tunachokiona huwa tunakihukumu haraka kwa mwonekano wake. Na hapa tumekuwa tunakosea sana, mara zote hukumu zetu za haraka huwa siyo sahihi. Mara zote kitu kinavyoonekana kwa nje, tena kwa mara ya kwanza, sivyo kilivyo kwa ndani. Hivyo itatusaidia sana kuacha kuhukumu kile tunachoona, kukipokea kama kilivyo na kuchukua muda kukijua kwa undani kabla hatujahukumu.
Vitu hivi viwili ni asili kwetu, hivyo tumeshazoea kuvifanya. Hivyo tunahitaji kufanya kazi ya ziada kuondoa mazoea haya. Kuna wakati utasukumwa sana kusema kitu, lakini kufanya hivyo siyo sahihi, hivyo lazima ujizuie kufanya hivyo. Pia kwa kila utakachokiona kwa mara ya kwanza utajikuta umeshakihukumu, futa hukumu yako mara moja na kuwa na mtazamo wa wazi katika kuangalia kitu hicho.
Kusema sana kunakuingiza kwenye matatizo, na kuhukumu kila kitu kunakunyima fursa nzuri zaidi. Jidhibiti kwenye maeneo hayo mawili na utakuwa na maisha tulivu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,