Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu cha THE WAR OF ART; Winning the Inner Creative Battle kilichoandikwa na STEVEN PRESSFIELD. Kwenye kitabu hiki tunakwenda kujifunza jinsi ya kuishinda vita inayoendelea ndani ya kila mmoja wetu na kumzuia asifanye makubwa, hasa kupitia ubunifu.

war of art

Utangulizi Wa Kitabu Na Kuhusu Mwandishi.

Steven Pressfield (kuzaliwa 1943) ni mwandishi wa vitabu, riwaya na historia wa nchini Marekani. Ameweza kuwa mwandishi mashuhuri kupitia riwaya zake ambazo ni The Legend of Bagger Vance, Gates of Fire, Tides of War na Last of the Amazons.

Vitabu vyake visivyo vya riwaya ambavyo vimefanya vizuri sana ni The War of Art: Break Through the Blocks and Win Your Inner Creative Battles, Do The Work, The Warrior Ethos na Turning Pro.

Kabla ya kukubali kusudi lake la uandishi, Steven alifanya kazi nyingi lakini zote hazikumridhisha. Baadhi ya kazi alizowahi kufanya ni mwandishi wa matangazo, mwalimu wa shule, mwendesha malori, muuza baa, mhudumu kwenye hospitali ya magonjwa ya akili na mwandishi wa skrini. Baada ya kugundua anachopenda zaidi ni uandishi, aliamua kuachana na mengine yote na kufanya uandishi pekee. Japo mwanzoni alipitia magumu, ikiwepo kukosa pa kuishi, lakini uvumilivu na kujituma kumeweza kumfikisha kwenye mafanikio makubwa.

Kwenye kitabu hiki cha The War of Art Steven anatushirikisha safari yake ya uandishi, jinsi alivyokuwa anakwepa kuingia kwenye uandishi na jinsi alivyoingia na kuweza kufanikiwa.

Steve anatuambia kwamba kuna adui mkubwa ambaye anatuzuia sisi tusifanye kazi za kibunifu tunazotaka kufanya. Iwe ni uandishi, uchoraji, uimbaji, uigizaji na hata ujasiriamali, kila tunapopanga kuanza, zinatokea changamoto mbalimbali.

Steve anatuambia adui huyu anayetuzuia ni UKINZANI wa ndani (INTERNAL RESISTANCE), kwa maneno mengine, adui wa sisi kupiga hatua ni sisi wenyewe, tunaweza kuwalaumu wengine na hata mazingira, lakini Steve anatuonesha kwamba tatizo linaanzia ndani yetu wenyewe.

Kitabu hiki cha The War of Art kimegawanyika kwenye sehemu tatu.

Sehemu ya kwanza Steve anatuonesha dalili za ukinzani, hapa tunatona jinsi ambavyo mambo tuliyozoea kuyafanya yamekuwa yanatuzuia kufanya kazi zetu za kibunifu.

Sehemu ya pili Steve anatupa mbinu za kushinda ukinzani uliopo ndani yetu. Hapa tunaondoka na hatua za kwenda kuchukua ili tusizuiwe na chochote katika kufanya kazi zetu za kibunifu.

Kwenye sehemu ya tatu Steve anatushirikisha maisha ya juu, maisha ya kiroho ambayo hayasumbuliwi na ukinzani. Steve anatuonesha kwamba mfanyaji wa kazi ya sanaa, iwe ni mwandishi, mwigizaji au mjasiriamali, yeye ni chombo tu kinachotumika kufikisha ujumbe ambao tayari upo. Sehemu hii ya tatu ni ya kiroho zaidi na inayotujengea msingi imara katika kazi zetu za kibunifu.

Karibu sana kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha The War of Art uweze kushinda ukinzani uliopo ndani yako na kufanya makubwa kupitia ubunifu ambayo tayari unao.

Ratiba ya siku ya Steven Pressfield.

Steven anatushirikisha ratiba yake ya siku kama ifuatavyo;

Anaamka asubuhi, anaoga na kupata kifungua kinywa. Baada ya hapo anasoma gazeti na kama kuna simu za kupiga anafanya hivyo. Anakunywa kahawa na kuvaa nguo zake za bahati ambazo huwa anazivaa anapoandika na kuelekea ofisini. Akifika ofisini anawasha kompyuta na kuweka vizuri mazingira ya ofisi yake na kisha kufanya sala yake maalumu aliyojifunza kutoka kwenye kitabu cha Odyssey cha Homer, sala hii ni ya kuamsha roho ya uandishi (Muse).

Anaanza kuandika saa nne na nusu na anaandika bila kuacha mpaka pale anapoanza kuandika makosa mengi, anajua hapo amechoka na anafunga kazi. Hapo anakuwa ametumia masaa kama manne kuandika. Anahamisha kazi yake aliyoandika kwenda kwenye flash disk na kuzima kompyuta. Hapo inakuwa ni saa tisa mchana, anafunga ofisi na kuondoka.

Steve anasema hajali ameandika kurasa ngapi wala hajali kama ameziandika vizuri, bali anachojali ni ameweka muda wake kwenye uandishi na kutoa kila kilichokuwa ndani yake. Hilo tu ndiyo muhimu kwa siku hiyo.

Anachojua Steven Pressfield.

Steven anatuambia kuna siri ambayo waandishi wabobezi wanaijua ambayo waandishi wachanga hawaijui. Na siri hiyo ni hii; kilicho kigumu kwenye uandishi siyo uandishi wenyewe, bali kukaa chini na kuandika. Kinachotuzuia tusikae chini na kuandika ni ukinzani.

Aina mbili za maisha.

Steven anatuambia kwamba kila mmoja wetu ana aina mbili za maisha.

Aina ya kwanza ni maisha tunayoyaishi kila siku, haya ni yale maisha ya mazoea ambapo unafanya mambo ya kawaida yanayofanywa na wengine.

Aina ya pili ni maisha ambayo hujayaishi, maisha haya ni yale ambayo ni halisi kwako, yanayoleta mchango wako wa tofauti. Wengi huwa hawaishi maisha haya kwa sababu ni ya tofauti na magumu.

Steve anatuambia kinachosimama kati ya maisha tunayoishi na yale maisha halisi ambayo hatujayaishi ni ukinzani.

Steve anatuonesha jinsi ambavyo huwa tunakuwa na nia njema kabisa ya kufanya kitu, tunachukua hatua za awali za kufanya kitu hicho, lakini badaye hatuendelei. Labda umepanga kufanya mazoezi, unanunua kabisa vifaa ya mazoezi, lakini baada ya siku chache za mazoezi huendelei tena. Nia yako ya kwanza ndiyo maisha ambayo hujayaishi, na kinachokufanya usiyaishi ni ukinzani uliopo ndani yako.

Ukinzani ndiyo sumu yenye nguvu kubwa duniani. Ndiyo mzizi wa kukosa furaha, umasikini, magonjwa na matatizo ya kila aina. Ukinzani huwa unatuangusha kiroho na kisha kututawala, kutuzuia tusifikie uwezo mkubwa ulipo ndani yetu. Unapaswa kutangaza ukinzani kuwa uovu ili uweze kupambana nao na kuishi maisha halisi kwako.

Ukinzani unamwathiri kila mtu katika kipindi fulani cha maisha yake. Wachache wanaoweza kuvuka ukinzani huo ndiyo wanaishi maisha halisi kwao. Wengi wanashindwa kuishi maisha yao kwa sababu ukinzani unawashinda. Ukinzani ni mgumu kuushinda kwa sababu una nguvu kubwa kuliko treni huku ukiwa na kasi kuliko risasi.

Tumekuwa tunasikia hadithi za mtu ambaye amekutwa na ugonjwa wa kansa na kuambiwa ana miezi sita ya kuishi. Kwa kusikia habari hizo, mtu huyo anaacha kazi aliyokuwa anaifanya, anarudia ndoto yake ya uandishi na ndani ya miezi sita anakuwa amekamilisha kitabu na kwa bahati nzuri, kansa nayo inapotea. Hii inaonesha kwamba ili kushinda ukinzani, unahitaji kupitia mambo magumu na makubwa.

Ukinzani umekuwa unajificha kwenye sababu na tabia mbalimbali, mfano ulevi na uteja wa madawa ya kulevya, magonjwa mbalimbali, udaku, kuzurura mitandaoni, na mengine tunayofanya ili kupoteza muda na tusifanye yale muhimu kwa maisha yetu.

Steve anatuambia kama kila mtu ataweza kuyaishi maisha yake halisi, basi mambo haya yatatokea; washauri wote wa kisaikolojia watakosa kazi, magereza yatakuwa tupu, viwanda vya sigara na pombe vitafungwa, pamoja na viwanda vya vyakula vya haraka na vinavyotengeneza bidhaa za urembo. Biashara za burudani na starehe zitafungwa, makampuni ya madawa, hospitali pamoja na kada nyingi za afya zitapunguza sana wateja wake. Ukatili wa majumbani utaisha, uteja, unene kupitiliza, maumivu ya kichwa na hasira vyote pia vitaisha.

Ukisikiliza moyo wako kuna sauti fulani inakurudia mara kwa mara kuhusu nini unachopaswa kufanya. Lakini cha kushangaza umekuwa huisikilizi sauti hiyo, badala yake unaipooza kwa usumbufu mbalimbali. Hicho kinachokuzuia usisikilize sauti yako ni ukinzani, na kama utautambua na kupambana nao, utakuzika kabisa.

Adolf Hitler alipenda kuwa msanii, akiwa na miaka 18 alichukua urithi wake na kwenda Vienna kujifunza sanaa. Alisoma chuo cha sanaa na baadaye usanifu, lakini leo hii hatujawahi kuona kazi yake yoyote ya sanaa, kwa sababu ukinzani ulimshinda. Na kuruhusu kwake ukinzani kumshinda kukaleta maafa makubwa duniani. Ilikuwa rahisi kwa Hitler kuanzisha vita ya pili ya dunia, kuliko kukaa chini na kuchora. Hapa tunaona jinsi ukinzani ulivyo na nguvu kubwa, na madhara pia.

Kupata uchambuzi kamili wa sehemu zote tatu za kitabu hiki cha The War Of Art karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.