Katika changamoto hii ya covid 19 tunayopitia sasa, ni rahisi sana kuona mambo hayawezekani.
Hilo linapelekea kukata tamaa na kukosa nguvu ya kuendelea na mapambano.
Hivyo hicho ni kitu cha kwanza cha kupambana nacho, kuhakikisha kila siku unayo hamasa na nguvu kubwa ya kuendelea na mapambano, bila ya kujali matokeo uliyopata jana.

Njia rahisi ya kupata nguvu na hamasa hii kila siku, ni kuianza siku yako kwa ushindi.
Na ushindi huo unaupata kwa kuchagua kitu kimoja ambacho utakifanya kila siku ya maisha yako bila ya kuacha hata siku moja.
Haijalishi ni kitu kidogo kiasi gani, wewe panga na fanya na utaona nguvu yake.
Unapofanya kitu hicho kwenye siku yako, unakuwa na siku yenye ushindi, hivyo hata kama utakutana na magumu kwenye siku yako, unajua tayari uliianza siku hiyo kwa ushindi.

Mfano wa vitu unavyoweza kupanga kila siku na vikakupa ushindi wenye hamasa kubwa;
👉🏼Mazoezi ya viungo ya aina yoyote ile.
👉🏼Kuandika kwa namna yoyote, iwe ni kitabu, makala au tafakari ya siku yako.
👉🏼Kujifunza kitu kipya, kupitia kusoma, kusikiliza au kuangalia.
👉🏼Kuwasiliana na mtu mmoja kuhusu biashara au kazi yako, iwe ni mteja, mshirika n.k
👉🏼Kutandika kitanda chako.
Vitu ni vingi, wewe chagua kipi utafanya na kisha kifanye kila siku.
Ukishakifanya, weka alama mahali kwamba umefanya, kisha endelea na siku yako.
Na kila unapokutana na lolote linalokukatisha tamaa kwenye siku yako, jikumbushe kwamba hiyo ni siku ya ushindi na ulishashinda kwa kile ulichopanga kufanya kila siku na ukafanya.

Anza na zoezi hili leo, kwa kuchagua nini cha kufanya, na kesho anza kufanya.
Ni vyema ukafanya asubuhi na mapema, ili unapoendelea na siku yako, unufaike na ushindi ulioanza nao.
Mapambano yanaendelea na kwa hakika tutavuka pamoja.
Kocha.