Una maoni gani kuhusu jua kuchomoza kesho? Ni swali ambalo mtu akikuuliza huwezi hata kupoteza muda wako kujisumbua nalo. Kwa sababu unajua haijalishi ni maoni gani unayo, jua litachomoza kesho kama ambavyo limekuwa linachomoza. Kunaweza kuwa na wingu ambalo litakuzuia usilione jua moja kwa moja, lakini uwepo wa mwanga utajua jua limechomoza.

Hii ni kutaka kukuambia kitu kimoja, maoni huwa hayabadili ukweli. Maono ni njia ya kujifurahisha kwa namna tunavyotaka wenyewe, lakini ukweli huwa unabaki kuwa ukweli.

Hivyo jukumu lako kwenye kila hali ni kutafuta kuujua ukweli, achana na maono, iwe ni yako au ya wengine, hayana msaada wowote. Kitakachokusaidia ni ukweli, na kwa kila jambo, kuna ukweli, ambao mara nyingi huwa umejificha au unaumiza hivyo watu hawapendi kuuangalia.

Una maoni gani kuhusu kifo? Hilo wala halihitaji maoni, ukweli ni kwamba kila mtu atakufa, lakini kabla hujafikia siku hiyo ya kufa, wajibu wako ni kuishi vizuri leo, kwa sababu huenda ndiyo ikawa siku ya mwisho kwako.

Una maoni gani kuhusu fedha? Unaweza kujikusanyia maoni mengi upendavyo, lakini ukweli ni kwamba fedha ni zao la thamani, ukitaka kupata fedha zaidi, toa thamani zaidi. Ukipeleka nguvu zako kwenye kutoa thamani zaidi na kuacha kukimbizana na kila aina ya maoni, itakusaidia sana.

Una maoni gani kuhusu madeni? Jiambie utakavyo, lakini ukweli ni kwamba, matumizi yako ni makubwa kuliko kipato chako. Hivyo una mambo mawili ya kufanya, kuongeza kipato chako na kupunguza matumizi yako.

Kwa kila tatizo au changamoto unayopitia, kuna maoni mengi utajipa na kupewa na wengine, lakini hayo ni njia ya kujilevya tu. Angalia ukweli uko wapi na simama kwenye ukweli huo.

Maoni hayabadili ukweli.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha