Kama kuna kitu ambacho kinaweza kukusaidia sana lakini unakichukulia poa basi ni masikio yako. Masikio yako ni dhahabu, ni hazina inayoweza kukupa chochote kile unachotaka.

Hii ni kwa sababu, kila mtu huwa anaeleza wazi kile ambacho anataka au kutegemea kupata. Hivyo kama utakuwa mtu wa kusikiliza vizuri, utawaelewa watu vizuri na hivyo utaweza kuwashawishi wakupe kile unachotaka.

Unapokuwa unaongea na mtu, sikiliza kwa umakini mkubwa sana. Fungua masikio yako na sikia kile ambacho mtu anasema kwa mdomo wake. Na pia fungua macho yako kuona kile ambacho mtu anakisema kwa mwili wake. Maana mwili unasema kwa sauti kubwa kuliko hata mdomo unavyosema.

Muangalie mtu anapoongea, itikie na onesha vitendo mbalimbali kwa mtu kwamba unasikiliza na pia uliza maswali mbalimbali ili kumfanya mtu ajieleze zaidi.

Usikatishe mtu anapoongea kama hakuna umuhimu wa kufanya hivyo. Na pia usikimbilie kumjibu mtu anapokuwa amemaliza kuongea. Jipe sekunde chache kabla hujamjibu mtu unayeongea naye.

Unapokuwa unaongea na mtu, unapaswa kusikiliza kwa namna ambayo mtu huyo atajiona ndiye mtu pekee wa muhimu kwako hapa duniani kwa wakati huo. Na hapo mtu atakuwa tayari kufunguka.

Hili lina msaada kwenye kila eneo la maisha yetu.

Lakini kwenye biashara, hasa kwenye mauzo, lina msaada mkubwa zaidi. Watu wengi wamezoea kwenye mauzo kuwa wanaongea zaidi kuliko wateja. Lakini unapompa mteja nafasi kubwa ya kuongea, atakueleza shida zake zote, wasiwasi wake na hata kinachomkwamisha. Hiyo inakurahisishia wewe kujua maeneo gani ya kutolea ufafanuzi ili mteja aweze kufanya maamuzi ya kununua.

Masikio yako ni dhahabu, sikiliza na utapata nafasi ya kujua kwa kina kile ambacho mwingine anaeleza na uweze kuchukua hatua sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha