Huwa tunaanza kufanya kitu huku tukiwa hatujui mbele tunakwenda kukutana na nini.

Ni mpaka tunapoanza kufanya ndiyo tunakuja kukutana na magumu na changamoto ambazo kabla hatujaanza hatukuzitegemea.

Lakini kwa kuwa tumeshachagua kufanya, tunaendelea kufanya, na baadaye tunapata mafanikio ambayo hatukutegemea kupata.

Ukiangalia kwa nje au kwa mtu mwingine, ni rahisi kuona alijua anakwenda kupita wapi mpaka apate anachotaka. Lakini ukiangalia kwa ndani, kila mtu alipita maeneo ambayo hakutegemea kupita.

Kinachotuwezesha kuanza hata kama hatujajua tunaenda kupita wapi na pia kuendelea kwenda licha ya kupitia magumu, ni matumaini ambayo tunakuwa nayo.

Tunapokuwa na matumaini kwamba tutafanya makubwa na kupata matokeo makubwa, tunapata msukumo wa kuendelea kufanya hata pale tunapokutana na yale ambayo hatukuyategemea.

Hii ni kusema kwamba, wanaofanikiwa na wanaoshindwa, wanaweza kutofautishwa na matumaini waliyonayo. Mtu yeyote ambaye hana matumaini, hatapata msukumo wa kuanza na hata kuendelea na safari ya mafanikio, hasa baada ya kukutana na yale ambayo hakutegemea.

Pia hili linatufundisha kwamba, huhitaji kuwa na uhakika wa kila kitu ndiyo uanze, kwa sababu ukisubiri uhakika huo hutaupata. Na haka mtu angeweza kukuonesha uhakika huo, ukaona jinsi utakavyopitia magumu, huenda usingeianza safari.

Hivyo tujenge matumaini yetu, tuwe watu wa imani na tuishi kwenye wakati uliopo, kwa kuangalia kipi cha kufanya sasa hivi na siyo kutishika na yale yanayokuja. Hakuna yeyote mwenye uhakika wa kesho, hivyo kuruhusu ikusumbue ni kujikwamisha. Ila kila mtu anaweza kuchukua hatua sahihi leo, ambazo zitasaidia kesho iwe bora zaidi. Fanya hivyo kwa matumaini.

Mwisho kabisa, matumaini siyo mkakati, hivyo usiache kuwa na mkakati kwa sababu unaamini matumaini yatakuvusha. Matumaini ni kichocheo tu, bali unachofanya unahitaji mkakati sahihi unaoufanyia kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha