“He who is looking for wisdom is already wise; and he who thinks that he has found wisdom is a stupid man.” —EASTERN WISDOM

Yule aliye tayari kujifunza kila wakati ndiye mwenye hekima,
Lakini yule ambaye anafikiri tayari ameshajua kila kitu ni mpumbavu.
Ujuaji umewakwamisha wengi sana,
Hasa kwa zama hizi za taarifa na maarifa ambapo mambo yanabadilika kila siku.
Wengi wanashindwa kwenda na kasi ya mabadiliko na kuishia kuachwa nyuma.
Kila siku, ni siku yako ya kujifunza, kuwa tayari kwa hilo na tafuta fursa za kulifanyia kazi.
Unapokutana na mtu ambaye ana kitu ambacho wewe huna au amepiga hatua ambazo wewe hujapiga, basi jua kuna kitu anajua ambacho wewe hujui.
Badala ya kujifanya unajua sana, kuwa mnyenyekevu na jifunze kwake.
Kama kuna kitu hujui uliza, utaonekana mjinga kwa dakika chache lakini utakuwa umejua.
Ila usipouliza, siyo tu unabaki kuwa mjinga milele, bali unakuwa mpumbavu,
Maana mjinga anajua hajui, lakini mpumbavu hajui kwamba hajui, hivyo anaamini anajua kila kitu.
Hakuna awezaye kujua kila kitu kwenye hizi zama,
Ndiyo maana kujifunza ni jambo ambalo haliwezi kuwa na mwisho.
Tumuige Socrates, ambaye alisema kama anaonekana ni mtu mwenye hekima kuliko wote, ni kwa sababu anajua hakuna anachojua.
Ukiwa na mtazamo huo, utajifunza mengi mno na wengi watakuwa tayari kukufundisha wanayojua.
Lakini ukiwa na mtazamo wa kujua kila kitu, hutajifunza na wengine watakwepa kukufundisha.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania