Mara nyingi yule anayefanya kitu huwa anasahau, lakini yule anayefanyiwa huwa hasahau.

Hili lipo zaidi kwa yale mambo ambayo yanaibua hisia kali kwa wale wanaofanyiwa, iwe ni hisia chanya za upendo na furaha au hisia hasi za hofu, chuki na huzuni.

Unapaswa kuwa makini sana na kila unachowafanyia wengine, ukijua kwamba wewe utasahau, lakini wao hawatasahau kamwe.

Ukimsifia mtu, wewe utasahau, lakini yule uliyemsifia hatosahau kamwe.

Ukiwa mwema kwa wengine unaweza kusahau, lakini wale unaowatendea wema hawatasahau kamwe.

Kadhalika unapowaumiza wengine, wewe unaweza kusahau, ila wale unaowaumiza, hawatakusahau kamwe.

Kwa kujua hili, kazana kufanya matendo yako yawe na manufaa kwa wengine, na hapo utaboresha sana mahusiano yako na wengine.

Jijengee tabia ya kuwa mwema kwa kila unayekutana naye, bila ya kujali ni nani au amefanya nini. Kwa njia hii utafanya maisha ya wengine kuwa bora na hawatakusahau kamwe.

Muhimu ni usifanye kwa kuigiza, bali fanya kwa nia ya kweli kutoka ndani yako, na utagusa maisha ya wengine kwa namba ambayo watakuwa tayari kutenda wema kwako pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha