“The salvation of mankind depends upon independent thinkers directing their thoughts rightly.” —RALPH WALDO EMERSON

Ukombozi wetu sisi binadamu upo kwenye fikra zetu,
Hivyo bila ya watu kuwa huru kufikiri na kupeleka fikra hizo sehemu sahihi, wataishia kuwa watumwa kwa watu wengine.
Na hiki ndiyo kinachoendelea sasa,
Watu wameacha kabisa kufikiri kwa akili zao wenyewe,
Na wameamua kufuata kundi, kuiga kile ambacho wengine wanafanya.
Jamii nayo inakazana kutengeneza watu ambao hawafikiri kwa uhuru, badala yake wanafikiri kama walivyotengenezwa.
Hivyo wanatengenezewa mazingira yanayowanyima uhuru wa kufikiri.
Badala ya mtu kufikiri huru kama mtu, atafikiri kama Mkristo au Muislamu, atafikiri kwa kabila lake, au kwa taaluma yake n.k.
Na ndiyo maana watu wengi wanajikuta kwenye changamoto zinazofanana, kwa sababu fikra zao ni sawa.

Akili yako ina uwezo mkubwa sana,
Na njia pekee ya kufikia na kutumia uwezo huo, ni kufikiri kwa uhuru.
Kuiruhusu akili yako kufikiri bila ya kuangalia kile kilichopo au pale ulipo sasa.
Kwa kufanya hivi, akili yako itakupa majibu mazuri na yatakayokusaidia sana.
Akili yako inajua ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako, lakini hujawahi kufikiri kwa uhuru ukajua.
Akili yako inajua nini unaweza kufanya kwa utofauti kabisa na wengine, lakini hujawahi kufikiri na kuisikiliza.
Badala yale unaruhusu fikra za wengine zikutawale.

Utumwa wa zamani ulikuwa ni wa mwili, watu walifungwa miili yao na kutumiwa kuzalisha, huku wakiumizwa miili yao kama hawakutii.
Utumwa wa sasa ni wa fikra, watu wamefungwa fikra zao ili kufanya kile chenye manufaa kwa wengine, na mtu anapokataa kutii, anaumizwa kiakili, ndiyo maana magonjwa ya akili kama msongo, sonona na hata uteja yanakua kwa kasi sasa.

Unahitaji uimara kwa kiakili ili uweze kuvuka utumwa huu wa kifikra ambao umewatawala wengi.
Unapaswa kukataa kabisa kufikiri kama wengine wanavyotaka, na kuhakikisha fikra zako zinakuwa huru.
Simama kwenye kile ambacho ni sahihi kwa wote, hata kama wengine wanaona siyo sahihi.
Unapokuwa huru kufikiri, unajikomboa wewe na wengine pia.
Hebu anza sasa kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani yako,
Na utaweza kufanya makumbwa mno.
Maana kila aliyewahi kufanya makubwa hapa duniani, alikuwa huru kufikiri licha ya kupingwa na wengine wengi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania