“I was made for the library, not the classroom.The classroom was a jail of other people’s interests. The library was open, unending, free.” — Ta-Nehisi Coates

Unapokuwa shuleni, haupo huru kujifunza yale unayotaka kujua kwa kina,
Badala yake utapangiwa ni maarifa ya aina gani upate,
Na kwa kuwa unapimwa kwa mtihani, basi lengo kuu la kusoma inakuwa kufaulu kwanza mtihani na siyo kupata maarifa kwa kina.
Hii inafanya elimu rasmi iwe gereza, ambapo unalazimika kufanya vile ilivyoandaliwa.

Lakini nje ya darasa, kuna njia nyingine nyingi za kupata maarifa, ambazo ni huru kabisa.
Maktaba zote ambazo zina vitabu vya kila aina, hakuna anayekupangia ni maarifa gani unapaswa kuyapata.
Hivyo uko huru kuchagua nini ujifunze na kwa kiwango gani.
Hakuna mtihani ambao utakulazimisha upate maarifa ya aina fulani.
Upo huru kabisa kujifunza kile unachotaka.

Lakini cha kushangaza sasa, ni namna watu wanavyochukulia hili.
Wakiwa shuleni wanakazana kusoma yale wanayopangiwa ili wafaulu mtihani.
Wakimaliza masomo hawajifunzi tena.
Halafu utawakuta wakilalamika kwamba maisha yao ni magumu na hawana uhuru.
Utakuwaje huru wakati unang’ang’ana na yale uliyofundishwa kwenye jela ya maarifa?
Umefika kwenye uhuru wa kujifunza utakacho, lakini huutumii.

Tutumie vizuri uhuru tulionao baada ya kuondoka shuleni,
Uhuru wa kujifunza chochote tunachotaka,
Na kwa maktaba ambazo tunaweza kutembea nazo muda wote kupitia simu zetu.
Chagua ni kitu gani unachotaka kujifunza kwa kina,
Kisha chagua vyanzo sahihi kwako kupata maarifa,
Halafu pata maarifa hayo, kwa namna ambayo yatakusaidia kupiga hatua kwenye maisha yako.
Kuna maarifa na taarifa nyingi, usipojua unachotaka na ukachagua kwa usahihi, utapotezwa na wingi huo wa maarifa na taarifa.

Mwisho kuwa makini sana na udhaifu ambao binadamu tunao.
Tunapokuwa kwenye utumwa/kifungo huwa tunapambana sana kupata uhuru.
Lakini tunapopewa uhuru, tunakazana kurudi tena kwenye utumwa/kifungo.
Wewe upe uhuru heshima yake, kwa kuutumia inavyostahili.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania