Jamii yetu kwa sasa kama vile imevurugwa katika malezi ya watoto, watoto wengi wanaozaliwa katika karne hii asilimia kubwa wanaoishi mijini na wanaofanya kazi wanasaidiwa malezi na wasaidizi wa kazi. Wasaidizi wa kazi tunaowaachia watoto nao hawana hata ujuzi wowote wa kulea, hivyo tukishampata na kumwachia mtoto atajua yeye vile anavyolea ili mradi tumepata mtu wa kutusaidia kukaa na mtoto.

Huwa hatupimi je huyu tunayemwachia mtoto ametokea wapi, tabia yake ikoje tunakuja kushtuka baadaye kabisa pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo. Sasa ili watoto wetu wakue katika malezi bora tunaalikwa kufanya nini?

Liko jawabu moja ambalo ni ushirikiano wa wazazi. Malezi ya watoto ni kazi kama zilivyo kazi nyingine,na kama ulikua unachukulia poa na kuona kama kazi ya malezi ni ya kina mama pekee yake au wadada basi unakosea, malezi yanahitaji ushirikiano mkubwa sana katika ya baba, mama na mtoto. Bila ya wazazi kuwa na ushirikiano hakika hutoweza kuwa familia yenye malezi bora.

Jinsi mafiga yaliyo na yanavyofanya kazi ndivyo wazazi na mtoto mnatakiwa kuwa, mmoja akikosekana maana yake mambo hayawezi kwenda vizuri. Kama ni kupika huwezi kupika ukiwa na figa moja au mawili lazima uwe na matatu kwanza.

Wazazi wengine hawajui hata watoto wanaendeleaje, wanapitia nini yeye anachokiangalia ni yeye tu. Watoto wanahitaji ufuatiliaji wa hali ya juu na kwenye ufuatiliaji bila kuwa na ushirikiano kati ya mzazi na mtoto malezi yanakuwa magumu.

Kila mzazi awe na muda na mtoto wake, baba au mama unatakiwa kuwa na muda na watoto wako ujue wanaendeleaje na nini wanapitia. Watoto huwa wanakua wanabadilika tabia sasa usipojua wanaendeleaje huwezi kujua wanapitia nini kwenye maisha yao. Lakini unapokuwa una muda nao lazima utajua kile wanachopitia.

Kila mzazi atumie nafasi yake vizuri kuhakikisha anatimiza wajibu wake kadiri ya nafasi yake. Familia yenye umoja lazima iwe na ushindi na wazazi ambao wanashirikiana katika malezi ya watoto lazima watoto watakua vizuri sana ila kama wazazi hawana ushirikiano kila mtu anakua yuko bize na mambo yake kamwe hamwezi kupata ushindi wa kuwa na familia bora.

Watoto nao huwa wana mtindo wa kucheza na akili za wazazi, wakiona wazazi wako makini wanafuatilia kwa karibu nao wanajijengea nidhamu ya kufanya kile walichoambiwa. Hivyo mjenge mtoto katika malezi ambayo hayatakuja kukusumbua baadaye. Shirikiana na mwenzako katika malezi kama vile mlivyoshirikiana na mwenzako kupata watoto au mtoto ambaye mnaye, usimtegee mwenzako bali weka kazi.

Hatua ya kuchukua leo; wazazi au walezi shirikianeni katika kuwalea watoto vizuri kwani malezi ya watoto siyo ya mtu mmoja bali wazazi wote wawili. Usipojitoa katika malezi ya watoto wako maana yake umechagua kuwekeza sehemu yenye hasara na tegemea kupata hasara na unapowafundisha usiwafundishe kwa ukali bali kwa lugha ya upendo.

Kwahiyo, watoto wako ni mbegu uliyoipanda, unatakiwa uifuatilie mbegu hiyo uliyoipanda mpaka pale itakapokua. Inapohitaji kuhudumiwa ili ikue vizuri tafadhali wajibika, mbegu ambazo zinapandwa na kuacha huwa hazikui vizuri. Ila zile ambazo zinakuwa zinafuatiliwa kuanzia kupandwa yaani kutungwa kwa mimba mpaka mtoto anazaliwa wanakuwa wako vizuri sana. usikubali kufanya uwekezaji wa hasara bali wekeza uwekezaji wenye faida kwako na jamii kwa ujumla.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana