“You should look in suffering for the seeds of your future spiritual growth, or the bitterness of suffering will be severe.” – Leo Tolstoy

Unapopitia magumu na mateso kwenye maisha yako,
Una njia mbili za kuyaangalia.
Unaweza kuyaangalia kama kitu kibaya kinachokuja kukuumiza, na kwa namna hiyo mateso hayo yanakuwa mabaya zaidi kwako.
Au unaweza kuyaangalia kama kitu kizuri kinachokuja kukukuza zaidi na hapo mateso hayo yanakuwa mazuri kwako.

Ni kanuni ya asili kwamba mazingira yanapokuwa magumu, viumbe waliopo kwenye mazingira hayo hufuata moja ya njia hizo pili,
Huwa imara zaidi na kuyamudu mazingira hayo magumu (survival)
Au hufa kwa kushindwa kuyamudu mazingira hayo magumu (perish)
Mazingira yetu sisi binadamu yanapokuwa magumu, kinachoathirika ni roho zetu,
Zinaweza kuwa imara zaidi na kuweza kukabiliana na mateso tunayopitia na kupiga hatua, hapo unakuwa na MATUMAINI.
Au unaweza kuwa dhaifu na kuacha mateso hayo yakupoteze kabisa, hapo unakuwa umekata TAMAA.

Ni njia ipi unachukua inategemea sana mtazamo ambao unao kabla hata hujakutana na mateso.
Kama upo kwenye kazi au biashara ambayo haikulipi vizuri, huku ikikuhitaji uweke juhudi kubwa sana, na bado matokeo unayopata siyo uliyotaka, unaweza kutumia hali hiyo kama msukumo wa kukua zaidi au kupotea kabisa.
Utakuwa zaidi kama ulikuwa na mtazamo chanya wa mafanikio, kama ulipenda sana kazi au biashara hiyo, na kama umejipanga kufanya kilicho sahihi mara zote bila ya kujali matokeo.
Utapotea kabisa kama ulikuwa na mtazamo hasi na wa kushindwa, kama hukupenda unachofanya, kama unachoangalia ni kile tu unachofanya.

Anza na mtazamo sahihi na huo utakufanya uwe imara kila wakati, bila ya kujali ni nini unapitia kwenye maisha yako.
Miti miwili inaweza kuwa eneo moja, mmoja ukakua na mwingine ukafa.
Watu wawili wanaweza kuwa kwenye kazi au biashara moja, mmoja akafanikiwa na mwingine kushindwa kabisa.
Tofauti ya anayefanikiwa na anayeshindwa haitoki nje, maana wote wana mazingira sawa, bali inaanzia ndani, ule mtazamo walionao.

Tupambane kujijengea mtazamo sahihi kwenye maisha na kila tunachofanya,
Na haijalishi tunapitia magumu na mateso kiasi gani,
Hatutatetereka, maana tunajua mateso hayo hayadumu milele,
Na baada ya mateso hayo, inakuja neema kubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania