Moja ya vitu vinavyowazuia wengi kuanza yale waliyopanga kuanza, ni kuona bado hawajawa tayari.

Wengi wamekuwa wakiona bado hawajajifunza vya kutosha, au kuna kitu bado hawajajua, hivyo wanasubiri mpaka wajue kila kitu ndiyo waanze.

Huku ni kujidanganya na kuficha ukweli kwamba haujawa tayari kuanza.

Ukweli ni kwamba, tayari unajua kiasi cha kutosha kuweza kuanza na kama kuna ambacho hujui, utajifunza kwa kuanza kuliko kusubiri mpaka ujue ndiyo uanze.

Ukweli mwingine ni kwamba huwezi kujua kila kitu, hata ungesema upewe miaka 100 ya kujiandaa, kila siku maarifa mapya yanaongezeka, hivyo kama lengo ni kujua kila kitu kabla hujaanza, hutaanza. Unachohitaji ni kujua kiasi cha kuweza kuanza, ambacho tayari unajua, kisha kuendelea kujifunza kutokana na uhitaji.

Chochote unachojiambia bado hujawa tayari, iwe ni kuanza biashara, kuanza kuandika kitabu au kingine unachopanga, jua kabisa kwamba uko tayari, ni wewe kuanza na kuendelea kujifunza kadiri unavyokwenda.

Kinachotukwamisha siyo kwamba hatujui tunavyopaswa kufanya au hatujui wapi pa kuanzia kufanya, bali tunakosa utayari wa kuanza. Pale unapokuwa tayari kuanza, utaziona njia nyingi za kufanya unachotaka.

Chagua kile ambacho umekuwa unajiambia utaanza kufanya lakini huanzi, weka mpango wa kuanza kukifanya mara moja, anza kwa hatua ndogo na fanya kila siku, baada ya muda utaona matokeo ya tofauti kuliko kuendelea kusubiri.

Kama ni biashara, siyo lazima uanze kubwa, anza na bidhaa au huduma na tafuta wateja wa kuwauzia moja kwa moja, anza na mteja mmoja, mhudumie vizuri kisha mwombe awashirikishe wengine. Nenda hivyo na utajifunza na kupiga hatua kuliko kusubiri mpaka uweze kuanza biashara kubwa.

Kama unataka kuandika kitabu lakini unajiambia hujawa tayari, anza kwa kuandika maneno mia tano au elfu moja tu kwa siku, usijali ni maneno mazuri au mabaya, sahihi au siyo sahihi. Wewe sikiliza kile kinachotoka ndani yako na andika, kila siku bila kuacha hata siku moja, mahali pa miezi 6 mpaka mwaka, utakuwa umeandika maneno zaidi ya laki moja, hayo ukiyahariri vizuri, unatoka na kitabu kimoja bora kabisa.

Uko tayari kuanza, usijicheleweshe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha