Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu Zero to one: notes on startups, or how to build the future kilichoandikwa na bilionea mwekezaji Peter Thiel akisaidiwa na aliyekuwa mwanafunzi wake Blake Masters.

Kitabu hiki kinatupa mafunzo ya jinsi ya kuanzisha biashara mpya na itakayokuwa na mafanikio makubwa, biashara ya kipekee katika zama tunazoishi sasa ambapo biashara nyingi kubwa zinaigana na kushindana.
Kwenye kitabu hiki, Thiel anatuonesha kwa kina tofauti ya TEKNOLOJIA (TECHNOLOGY) ambayo anaita ni kutoka SIFURI kwenda MOJA na UTANDAWAZI (GLOBALIZATION) ambao anauita MOJA kwenda NAMBA KUBWA ZAIDI. Hapa Thiel anatuonesha mafanikio makubwa kwenye biashara yanakuja pale kunapokuwa na teknolojia mpya, yaani mtu anaanzia sifuri kwenda moja.
Thiel anatuambia kila fursa ya kibiashara huwa inakuja mara moja tu, baada ya hapo huwa haijirudii. Hivyo kama unataka kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara waliofanikiwa, usiangalie kile wanachofanya, bali angalia jinsi walivyofika kwenye kukifanya. Kama unataka kuanzisha mtandao wa kijamii, kumuiga Mark Zuckerbrrg aliyeanzisha Facebook hakutakusaidia. Bali kuangalia jinsi alivyoweza kuja na wazo la Facebook kutakusaidia.
Kuiga kile kinachofanywa na wengine ni rahisi kuliko kuja na kitu kipya, lakini unapoiga kinachofanyika, unajiweka kwenye ushindani mkali ambao utakusumbua. Lakini unapokuja na kitu chako kipya, na ukaweza kujitofautisha kwa namna ya kipekee, unaondokana kabisa na ushindani.
Kinachofanya biashara nyingi na hata makampuni makubwa kushindwa ni kukosa ugunduzi wa teknolojia mpya. Nyingi zinafanya mambo yale yale kwa namna bora zaidi, kitu ambacho wengine pia wanaweza kufanya na hivyo ushindani unakuwa mkali. Hivyo njia pekee ya mtu kujitofautisha biashara yako isife na kuondokana na ushindani ni kuwa na ugunduzi mpya kila wakati.
Kinachotutofautisha sisi binadamu na viumbe wengine ni uwezo wetu wa kutenda miujiza, uwezo wa kuja na njia mpya kabisa ya kufanya vitu. Miujiza hiyo tunayofanya wanadamu inaitwa teknolojia. Msingi wa teknolojia ni kuja na njia mpya za kufanya mambo kwa urahisi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Mfano ukiangalia upande wa usafiri, tulianzia kwenye kutegemea usafiri wa kutembea kwa miguu, tukaja usafiri wa kutumia wanyama, tukaingia kwenye meli na treni, baadaye magari na hatimaye ndege. Hivi ndivyo teknolojia imekuwa inarahisisha maisha yetu wanadamu.
Kwenye kitabu hiki cha ZERO TO ONE, mwandishi anatufundisha jinsi ya kujenga makampuni ambayo yanatengeneza vitu vipya. Anatushirikisha uzoefu wake kutoka makampuni aliyoanzisha ambayo ni PayPal na Palantir na pia kwenye makampuni makubwa ambayo ni mwekezaji kama Facebook na SpaceX.
Mwandishi anatoa tahadhari kwamba kitabu hiki hakina kanuni ya uhakika ya mafanikio. Anasema changamoto ya kufundisha ujasiriamali ni kwamba hakuna kanuni moja inayoweza kuwafaa watu wote. Hii ni kwa sababu ugunduzi ni kitu kipya na ambacho hakiwezi kutabiriwa au kutegemewa. Hivyo kitu pekee anachotufundisha ni jinsi ya kutafuta thamani kwenye kila eneo na kuacha kufikiria kwa kuiga na badala yake kufikiria kila kitu kwa upya.
KUHUSU WAANDISHI.
Kitabu hiki ni matokeo ya kozi ambayo Peter Thiel alifundisha kwenye chuo cha Stanford kuhusu kuanzisha biashara (Startup) mwaka 2012. Blake Masters alikuwa mwanafunzi kwenye darasa hilo na aliandika vizuri notisi za somo hilo na kuanza kuwashirikisha watu mtandaoni. Notisi hizo zilipata umaarufu kwa wengi kuzipenda na kuzidi kusambaa kwa kasi. Na hapo ndipo Peter Thiel aliposhirikiana na Blake Masters kuongezea notisi zile na kuwa kitabu hiki cha ZERO TO ONE.
Peter Thiel ni bilionea mjasiriamali na mwekezaji wa nchini Marekani. Mwaka 1998 yeye na wenzake walianzisha kampuni ya PayPal ambayo imekuwa inarahisisha utumaji wa fedha baina ya watu. Mwaka 2002 waliweka kampuni yao kwenye soko la hisa na baadaye kuiuza ambapo yeye na wenzake sita waliweza kuwa mabilionea. Mwaka 2004 alianzisha kampuni mpya inayoitwa Palantir ambayo ina teknolojia ya kuchakata taarifa mbalimbali za kiusalama.
Peter ni mwekezaji kwenye makampuni makubwa kama Facebook, SpaceX, LinkedIn, Airbnb na mengine mengi.
Blake Masters alikuwa mwanafunzi wa Stanford mwaka 2012 wakati Peter anafundisha darasa kuhusu kuanza biashara. Aliandika notisi ambazo zilisambaa sana mtandaoni ambazo zimekuwa chanzo cha kitabu hiki. Ni mwanzilishi mwenza wa kampuni inayoitwa Judicata, ambayo inafanya utafiti wa kiteknolojia kwenye sheria.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu cha ZERO TO ONE, ujifunze jinsi ya kufikiri tofauti, ili uweze kuja na ugunduzi mpya utakaokuwezesha kuwa na biashara ya kipekee na itakayokuwa na mafanikio makubwa.
CHANGAMOTO YA KESHO
Hakuna anayeweza kuitabiri kesho kwa uhakika wa asilimia 100. Lakini kuna vitu viwili kuhusu kesho ambavyo tuna uhakika navyo; moja kesho itakuwa tofauti na leo na mbili utafauti wa kesho utatokana na leo ilivyo. Kesho hapa haimaanishi siku ya kesho (tomorrow), bali wakati ujao (future). Kinachoamua matokeo ya wakati huo ujao ni hatua ambazo watu wanachukua katika wakati tulionao sasa. Kama watu hawatafanya vitu vya tofauti kwa miaka 100 ijayo, kesho mpya itakuwa umbali wa miaka 100. Lakini kama watu watafanya vitu vipya sasa, kesho mpya ipo karibu sana.
Tunapoifikiria kesho mpya, huwa tunaifikiria kwa maendeleo bora kuliko tuliyonayo sasa. Maendeleo hayo yanaweza kuwa ya mwendelezo, yaani kuboresha kile kilichopo sasa au ugunduzi mpya yaani kuja na kitu kipya kabisa. Maendeleo ya mwendelezo siyo magumu, kila mtu tayari anajua jinsi mambo yanavyofanyika. Lakini maendeleo ya ugunduzi ni magumu, kwa sababu yanamtaka mtu afanye vitu vya tofauti kabisa na vilivyozoeleka.
Kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa, maendeleo ya mwendelezo yanaitwa UTANDAWAZI, ambapo kile kinachofanya kazi eneo moja kinapelekwa eneo jingine. Mfano mzuri ni maendeleo ya taifa la China, yametokana na kuiga vile ambavyo vimefanya kazi kwenye nchi nyingine kama Marekani. Wachina wamekuwa wanaiga mifumo yote ambayo imekuwepo kwenye nchi zilizoendelea na hilo limewawezesha kuzalisha kwa wingi na kuleta ushindani mkubwa duniani.
Maendeleo ya ugunduzi kwa jina jingine yanaitwa TEKNOLOJIA. Mfano mzuri ni ukuaji wa haraka wa sekta ya TEHAMA kwenye eneo la Silicon Valley nchini Marekani, ambapo makampuni mengi mapya yameanzishwa kwenye sekta hiyo. Hii imefanya wengi kufikiria teknolojia inahusu TEHAMA pekee, lakini ukweli ni teknolojia inahusu kila eneo, na teknolojia ni pale mtu anapokuja na njia mpya ya kufanya kitu kwa urahisi zaidi.
Kwa muda sasa tumekuwa tunaishi kwenye maendeleo yanayotokana na utandawazi, ambapo nchi zinazoendelea zinaiga yale ambayo yalishafanywa kwenye nchi zilizoendelea. Lakini hili haliwezi kutusaidia kupiga hatua kama dunia kama hakutakuwa na ugunduzi mpya. Utandawazi unatengeneza ushindani ambao mwisho wake ni umasikini kwa wote wanaoshindana. Njia pekee ya kutengeneza mafanikio makubwa na utajiri ni kupitia teknolojia.
Tupo kwenye wakati ambao tunahitaji sana kuja na teknolojia mpya za kurahisisha maisha yetu. Karne ya 19 na 20 zilikuwa karne ambazo teknolojia ilikua kwa kasi sana duniani. Lakini kuanzia karne ya 21, maendeleo ya teknolojia yamekuwa machache, na mengi ni kwenye eneo la TEHAMA PEKEE.
Ukiangalia kwenye historia, teknolojia mpya haijawahi kutokea yenyewe, bali ililetwa na watu ambao walikuwa tayari kufikiri tofauti na kuja na njia bora za kufanya vitu. Hata baada ya kuja na njia hizo, watu hawakuzipokea, walizipinga kwa kuziona ni hatari. Mfano watu walikataa kupanda treni ya kwanza kwa kuamini kasi yake itafanya damu isimame. Watu walivunja mashine ya kwanza ya kushona iliyogunduliwa kwa kuamini itaharibu kazi zao.
Kwa kasi ambayo teknolojia ilikuwa inakwenda, wale walioishi karne ya 19 na 20, waliamini kufika karne ya 21 maisha yatakuwa bora sana. Waliamini muda wa watu kufanya kazi ungepungua, gharama za nishati kupungua na watu kuweza kusafiri kwenda matembezi mwezini na kwenye sayari nyingine. Lakini hayo hayajatokea, tumerudi nyuma kiteknolojia kuliko vizazi vilivyotutangulia.
Eneo pekee ambalo teknolojia imepiga hatua ni TEHAMA, na hapo ndipo kikwazo kikubwa cha teknolojia kilipoanzia. Ugunduzi wa simu janja (smartphone) na mitandao ya kijamii imesababisha usumbufu mkubwa kwa watu. Watu hawana tena umakini wa kuona mambo ambayo hayapo sahihi na yanayopaswa kubadilishwa kwa sababu umakini wao wote umetekwa na simu zao na mitandao ya kijamii.
Changamoto yetu kubwa leo ni kutengeneza teknolojia mpya ambazo zitaifanya karne ya 21 kuwa ya mafanikio makubwa kuliko karne ya 20. Kitu ambacho kinahitaji watu kujitoa, kufikiri kwa tofauti na kujaribu vitu vipya bila ya kuogopa au kujali wengine wanafikiri au kufanya nini.
Historia inatuonesha kwamba teknolojia mpya imekuwa inazalishwa na kikundi kidogo cha watu ambao wanafanya kazi pamoja (startup). Watu walio kwenye kikundi hicho wanakuwa na ushirikiano mkubwa na wana ndoto moja kubwa ambayo wanaifanyia kazi. Hili ni gumu kufanyika kwenye kampuni kubwa kwa sababu kuna ukiritimba mwingi. Watu kwenye makampuni makubwa wanachoangalia ni kupanda vyeo na kunufaika zaidi na siyo kujaribu vitu ambavyo vinaweza kushindwa.
Kwa upande wa pili ni vigumu kwa teknolojia mpya kuzalishwa na mtu mmoja anayefanya kazi peke yake. Mtu mmoja anaweza kufanya makubwa kwenye kazi za sanaa lakini siyo kuanzisha sekta mpya kiteknolojia.
Hivyo maendeleo ya teknolojia kwenye karne hii ya 21 yanategemea sana kwenye vikundi vya watu wachache wanaofanya kazi pamoja (startups). Kikundi hicho kinakuwa huru kufikiri tofauti na kujaribu vitu vipya hata kama vitashindwa.
Hapa ndipo Peter Thiel amewekeza nguvu zake, kusaidia kampuni hizo ndogo ndogo kufikiri na kujaribu vitu vipya. Amekuwa anazisaidia kampuni hizo kupitia uwekezaji na kupitia kitabu hiki, anazipa mwongozo ambao utawasaidia kuanzisha biashara zao na jinsi ya kuitengeneza kesho iliyo bora.
Kitabu hiki cha ZERO TO ONE, ni kitabu chenye msaada mkubwa kwa kila anayetaka kupiga hatua kwenye maisha yake kwa kuchagua kufanya vitu vipya na kujitofautisha na wengine. Karibu tujifunze ili tuweze kupiga hatua zaidi.
Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki pamoja na hatua za kuchukua ili uweze kujenga biashara bora na yenye mafanikio, ingia kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua; www.t.me/somavitabutanzania
Karibu sana rafiki yangu upate nafasi ya kujifunza kwa kina jinsi ya kuanzisha biashara ambayo itahodhi soko lake kitu ambacho kitakuondoa kwenye ushindani na kukupa mafanikio makubwa.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.