Tukiwa tunaendelea na msisitizo kwenye ufanyaji badala ya kupanga na kusubiri, kuna changamoto nyingine ambayo wengi wanaikaribisha.

Watu wengi huwa wanataka wafanye kila kitu wao peke yao, na hilo siyo tu linawakwamisha kuanza, bali pia linawafanya washindwe kuzalisha kitu bora na cha kipekee.

Huwezi kufanya kila kitu, huna muda wala nguvu za kuweza kufanya hivyo.

Unachopaswa kufanya ni kuchagua eneo ambalo utabobea na kisha kufanyia kazi hilo, na maeneo mengine tafuta watu watakaokusaidia au utakaoshirikiana nao.

Hakuna anayeweza kufanya kila kitu, lakini kila mtu anaweza kuchagua kitu anachoweza kukifanya vizuri na kikampa matokeo makubwa.

Anza kwa kuwa mtu sahihi kwenye kile unachochagua kufanya na kisha tafuta watu walio sahihi kwa kile ambacho huwezi kufanya na ushirikiane nao. Ukiwa sahihi, una nafasi nzuri ya kupata watu walio sahihi pia.

Muda na nguvu zako ni vitu ambavyo unavyo kwa uhaba, viwekeze na kuvitumia vizuri, kwenye yale unayoweza kuyafanya vizuri, yale yanayoweza kukutofautisha na wengine na kukujenga jina zuri, kisha mengine achana nayo, wape wengine wakusaidie.

Usitawanye sana muda na nguvu zako, bali elekeza kwenye maeneo muhimu na matokeo yake utayaona.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha