Tunaishi kwenye zama za usumbufu, zama ambazo ni vigumu sana kukaa kwenye ukimya na utulivu.
Kifaa tunachotembelea nacho kila mahali, yaani simu janja, hua hakitupi kabisa nafasi ya kuwa na ukimya na utulivu.
Kila wakati kinatuletea taarifa kwamba kuna watu wanatutafuta, kuna mambo yanaendelea mitandaoni na kadhalika.
Hivyo kila wakati tunahama kutoka hali moja kwenda nyingine, hatupati kabisa wakati wa kukaa kimya na kuwa kwenye utulivu.
Na hilo linachangia sana kwenye hali ya msongo ambayo wengi wanayo kwa sasa.
Unapaswa kujifunza kusikiliza ukimya wako, kwa sababu umebeba mengi unayoyahitaji.
Ni kwenye ukimya wako ndipo unapata nafasi ya kujijua wewe mwenyewe kwa undani.
Ukimya ndiyo unaokupa nafasi ya kuchakata yale yanayoendelea kwenye maisha yako, kujua yapi unapaswa kuyapa kipaumbele na yapi unapaswa kuyapuuza.
Unapokuwa katikati ya usumbufu, huwezi kuona umuhimu wa vitu kwa usahihi. Ni mpaka upate ukimya ndiyo unaweza kuona vitu kwa namna vilivyo.
Tenga muda kwenye siku yako ambapo utajiruhusu kwenda na hali uliyonayo, unapojisikia vibaya au uchoshi (kuboreka) usikimbilie kushika simu yako ili ujisikie vizuri, badala yake kaa kwenye hali hiyo kwa muda, na sikiliza kile ambacho hali hiyo inakueleza.
Akili zetu zina mambo mengi sana, na huwa zinatuweka kwenye hali fulani ili tupate nafasi ya kuzisikiliza. Lakini sisi tumekuwa hatuzisikilizi, tumekuwa tunakimbilia kwenye usumbufu ambao hautusaidii.
Wauzaji wa vitu mbalimbali wanajua udhaifu wetu tunapokuwa kwenye hali hizo, na ndipo huwa wanatumia muda huo kutushawishi kununua vitu mbalimbali, kwa ahadi kwamba tukishanunua tutajisikia vizuri. Tunawaamini, tunanunua, tunajisikia vizuri kwa muda mfupi, lakini baada ya hapo hali inarudi kama awali.
Usikubali kuingia kwenye mitego hiyo, jenga tabia ya kujisikiliza wewe mwenyewe na utaweza kujua kwa nini hujisikii vizuri na hatua sahihi kwako kuchukua ili kuondokana na hali hizo za kutokujisikia vizuri.
Jifunze kupumzika pale unapokuwa umechoka, kula chakula kizuri pale unapokuwa na njaa na kuuweka mwili wako kwenye mwendo kama njia ya kufanya mazoezi. Hivi ni vitu rahisi, vinavyokuunguka ambavyo ukivizingatia, utaepuka kuhangaishwa na mambo yasiyo muhimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,