Iko wazi kwamba kuendesha biashara ni kugumu na kuna changamoto nyingi. Lakini ugumu na changamoto nyingine tumekuwa tunaziongeza wenyewe, kwa yale tunayofanya au kushindwa kufanya.
Na moja ya maeneo ambayo tumekuwa tunaongeza changamoto kwenye biashara zetu ni kushindwa kutengeneza wateja wa biashara zetu.
Hii ni kwa sababu wengi huingia kwenye biashara bila ya kuwa na mkakati wowote wa kupata wateja. Wanachojua ni kwamba ukifungua biashara, na watu wakiiona basi watakuja kununua.
Lakini sote tunajua zama tunazoishi zina kelele na usumbufu mwingi, siyo rahisi mtu kujua kama upo na kuja kununua kama hujaweka juhudi za kumfikia na kumleta kwenye biashara.
Hapa kuna hatua tatu muhimu za kuchukua kwenye biashara ili kutengeneza wateja zaidi wa biashara hiyo. Ukifanyia kazi hatua hizi kila siku, biashara yako itakua kadiri muda unavyokwenda.
Hatua ya kwanza ni kuwafanya wateja wajue uwepo wako. Je wateja unaowalenga wanajua kwamba upo? Kwa sababu kama mteja hajui uwepo wako basi anajua haupo. Wajibu wako wa kwanza ni kumfanya mteja ajue uwepo wako, na hapa ndipo matangazo mbalimbali yanapohusika kwenye biashara yako. Na usihofu unaposikia matangazo, siyo lazima iwe kwenye tv, mitandao ya kijamii ni sehemu nzuri unayoweza kuitumia kutangaza. Kadhalika kwa kila unayekutana naye, hakikisha anajua unauza nini.
Hatua ya pili ni kuwashawishi wale wanaojua kuhusu biashara yako, wajaribu kuja kupata huduma kwenye biashara hiyo. Watu kujua uwepo wako pekee haitoshi, lazima uwe na njia ya kuwashawishi kuja kujaribu kile unachouza. Hapa pia unahitaji kuwa na vitu unavyofanya vitakavyowasukuma wateja kuja kukujaribu. Unaweza kutoa zawadi au ofa mbalimbali, ambazo zitamfanya mteja aone hana cha kupoteza kwa kuja kujaribu.
Hatua ya tatu ni kuhakikisha kila anayejaribu anarudi tena. Mtu atakuja kwenye biashara yako kwa mara ya kwanza kwa lengo la kujaribu, aone je yale aliyahidiwa yanapatikana kweli? Hivyo hakikisha hufanyi makosa kwenye hili, hakikisha unampa huduma ambayo hajawahi kupata popote ambayo itamfanya arudi tena na tena na tena. Mteja siyo yule anayenunua mara moja na asirudi tena, mteja ni yule anayenunua zaidi ya mara moja, na hata kuwaleta wengine pia.
Zingatia hatua hizo tatu na utaweza kutengeneza wateja zaidi kwenye biashara yako. Kila siku hakikisha unafanyia kazi hatua hizo, hakikisha kuna watu wapya wanajua kuhusu biashara yako, hakikisha kuna wanaoshawishika kujaribu na pia hakikisha wale waliojaribu wanarudi tena kununua.
Siyo zoezi gumu, ila linahitaji msimamo, subira na uvumilivu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,