Hakuna mtu ambaye kila kitu kinaenda kama alivyopanga kwenye maisha yake.
Lakini wapo watu wanaoendelea kufanikiwa licha ya kukutana na vikwazo vingi, huku wengine wakishindwa kwa vikwazo hivyo hivyo.
Wale wanaofanikiwa ni wenye mtazamo wa kutoruhusu chochote kiwe kikwazo kwa safari yao.
Wanachukulia safari ya mafanikio kama mchezo au onesho ambalo lazima liendelee, iwe kuna mvua au jua, giza au mwanga, mchezo unaendelea.
Mwanafalsafa wa Ustoa Epictetus kwenye moja ya mafunzo yake anatupa hadithi ya mstoa mwingine aliyeitwa Agrippinus, ambaye siku moja asubuhi alipewa taarifa kwamba amewekwa kizuizini na siku hiyo atapaswa kuondoka na kwenda Aricia ambapo atakuwa kizuizini. Jibu lake lilikuwa rahisi; hakuna tatizo, chakula cha mchana tutaenda kula Aricia.
Huu ni mtazamo ambao kila mmoja wetu anauhitaji, mtazamo wa mchezo lazima uendelee. Mtazamo wa kutokushtushwa na yale tunayokutana nayo, bali kuyatumia kwa mafanikio yetu makubwa zaidi.
Unapokutana na kile ambacho hukutegemea kukutana nacho, usiruhusu kwa namna yoyote kiwe kikwazo kwako. Badala yake kigeuze kuwa njia ya kufika kule unakotaka kufika.
Kama ambavyo mstoa mwingine Marcus Aurelius amewahi kutuambia, kikwazo kwenye njia huwa ndiyo njia ya kufika kule tunakotaka kufika.
Mtazamo wako kila wakati ni huu, mchezo lazima uendelee, angalia kila fursa iliyo mbele yako ya kuuwezesha mchezo kuendelea na itumie vyema.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha,kweli lazima mchezo uendelee/yaani maisha lazima yosonge mbele.ila kwa Elimu sahihi na mafunzo sahihi.
LikeLike
Hakika
LikeLike