Kitu kimoja ninachokiamini, na nitaendelea kuamini hivyo maisha yangu yote ni kwamba wale wanaosema hawana muda wa kufanya vitu fulani wanavyotaka kufanya huwa wanadanganya. Siyo kweli kwamba hawana muda, ila tu hawataki kufanya, sasa kwa kuwa hawataki kuukabili ukweli, wanatumia kisingizio cha muda.

Kwenye siku kuna masaa 24 ambayo ukiyageuza kwenda kwenye dakika, unapaa dakika 1440, je katika dakika hizo elfu moja mia nne na arobaini unakosa dakika kumi tu za kutenga kwa ajili ya kile muhimu kwako kufanya?

Najua utajiambia dakika kumi zinaweza kufanya nini?

Na jibu ni dakika kumi zinaweza kufanya mengi unayoahirisha sasa kufanya.

Unasema husomi vitabu kwa sababu huna muda, dakika kumi utakazoweka kwenye kusoma zitakuwezesha kusoma kurasa 5 mpaka 10, ukifanya hivyo kila siku kwa mwezi utamaliza kusoma kitabu kimoja, kwa mwaka vitabu zaidi ya 10, kitu ambacho kitakufikisha mbali kweli.

Unasema huandiki kwa sababu huna muda, dakika 10 zinakutosha kuandika maneno 300 mpaka 500 kulingana na kile unachoandika. Kama ni kitu unachopenda na unachokijua, unakuwa na mengi ya kuandika.

Unasema hufanyi mazoezi kwa sababu huna muda, ukiruka kamba ka dakika kumi tu, utakuwa umefanya zoezi kubwa mno, fanya hivyo kila siku na utajenga afya imara.

Kuna vitu vingi mno unaweza kufanya kwenye dakika kumi ulizozitenga na kuweka umakini wako kwenye kitu hicho, kufanya tahajudi, kuboresha mahusiano, kuboresha kazi yako na mengine mengi.

Unachohitaji siyo muda zaidi, bali umakini kwenye muda ambao tayari unao.

Hivyo chagua kama utaendelea kujidanganya huna muda, au kama utaamua kuanza kutumia muda ulionao vizuri. Maisha ni yako na chaguo ni lako, ila kumbuka unaweza kuwadanganya watu wengine wote, lakini huwezi kujidanganya wewe mwenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha