Kila mtu huwa ana dalili fulani za hofu, pale anapokuwa na hofu, mwili wake huwa unamsukuma kufanya kitu fulani, hata kama hajui. Kuna ambao hung’ata kucha, kuna ambao mikono hutetemeka na wengine kutokwa jasho, hata kama hakuna joto.
Ipo dalili ya kiakili ya hofu, ambayo huwa inawapata walio wengi, lakini huwa hawajui kama ni hofu. Wao wanaona ni kitu cha kawaida, lakini kwa uhalisia ni hofu.
Dalili hiyo ni kutaka kuongeza zaidi. Pale unapojikuta unataka kuongeza zaidi kwenye kile ambacho tayari umeshafanya hata kama umefanya kwa ukamilifu, jua hapo unasukumwa na hofu.
Mfano katika maongezi na mtu, umeshamweleza anachopaswa kujua, lakini unajikuta unatamani ungeongeza zaidi, hapo jua kuna hofu inakusukuma. Au unamuuzia mtu kitu, ameshachukua kitu hicho lakini unatamani ungeongeza zaidi hiyo ni dalili ya hofu.
Unakuwa unahofia watu hawajakuelewa au hawatakuthamini.
Hata kwenye vitu vya kawaida, unafikiri unahitaji nguo za aina ngapi, magari ya aina ngapi na vitu vingine vya aina hiyo. unapojikuta unahitaji zaidi hata kama ulivyonavyo vinakidhi mahitaji, msukumo mkubwa unakuwa ni hofu.
Hofu inakusukuma uone ukifanya zaidi au ukiwa na zaidi basi ndiyo utakuwa umekamilika, watu watakuthamini zaidi. Lakini hilo siyo sahihi.
Huwezi kuishinda hofu kwa kuongeza zaidi, kwani hilo litazidi kuchochea hofu hiyo. Njia pekee ya kuishinda hofu ni kujiamini, kujua kile ulichofanya au ulichonacho kinatosha. Unapaswa kutambua ni wakati gani zaidi inasababishwa na hofu na kutokukubali hofu iwe kitu kinachokusukuma.
Zaidi siyo dawa ya hofu, bora ndiyo dawa sahihi ya kile kinachokupa hofu. Achana na kukimbiza zaidi na weka nguvu kwenye kufanya kilicho bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,