Hivi ni vitu viwili unavyopaswa kuvifuata, unavyopaswa kujifunza na pale unapohitaji maoni au mrejesho, basi angalia kwenye vitu hivyo viwili.

Asili ina sheria zake ambazo huwa hazibadiliki kulingana na eneo au hali. Sheria za asili ni za kudumu. Ukizifuata utanufaika nazo, ukizivunja utaadhibiwa. Asili haijali wala haina huruma, inajua njia moja, ambayo ni njia yake.

Ni kanuni ya asili kwamba chochote kinachopatikana kwa wingi thamani yake huwa siyo kubwa. Kwa kujua na kuishi kanuni hii kila siku, unalazimika kufanya kile ambacho hakuna wengi wanaoweza kukifanya. Hapo ndipo utaweza kuthaminika zaidi na kupata mafanikio makubwa.

Kadhalika asili ni nzuri kwenye kupata maoni au mrejesho. Kama kuna kitu unataka kufanya lakini huna uhakika, angalia asili inafanyaje mambo yake. Kwa kuangalia asili, utajifunza njia bora ya kufanya chochote.

Soko pia ni njia nzuri ya kujifunza na kupata maoni au mrejesho.

Soko halijali nani anauza nini, ana uhitaji kiasi gani, bali linajali unalipa thamani gani. Unaweza kuwa una uhitaji sana wa fedha, ukawa huna hata fedha ya kula, hivyo unahitaji sana fedha, na hivyo ukapeleka sokoni bidhaa ambayo watu hawaitaki au hawaithamini. Hawatanunua hata kama utawaambia una uhitaji kiasi gani. Huku mwenzako ambaye hana uhitaji mkubwa wa fedha akiuza zaidi bidhaa ambayo watu wana uhitaji nayo.

Kama unataka kujifunza, angalia soko linaendaje, angalia watu wanathamini nini na wapo tayari kutoa kiasi gani kupata thamani wanayoitaka. Kwa kuliangalia soko, utajifunza mengi na yatakayokusaidia.

Pia unapotaka kupata maoni au mrejesho wa kitu, usiwaulize watu, maana watakujibu kile unachotaka kusikia. Cha kufanya nenda sokoni na bidhaa au huduma unayotaka kupata maoni au mrejesho, kisha anza kuwashawishi watu wanunue.

Ukiona watu wanakuwa tayari kununua, hasa wale wasiokujua kabisa, jua hapo kuna thamani. Lakini ukiona watu wanasita kununua, jua hapo hujawa na thamani sahihi, hivyo rudi ukatengeneze thamani zaidi.

Kwa kuingia sokoni, unapata majibu sahihi ya kile ambacho watu wapo tayari kulipia, kwa vitendo na siyo nadharaia.

Tutumie vitu hivi viwili kujifunza na kupata mrejesho, asili na soko, vitu hivi vina misingi yake ambayo ukishaijua na kuifuata, hakuna kinachoweza kukuzuia usipige hatua kubwa. Vunja misingi hiyo na hakuna hatua utakayoweza kupiga.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha