Kutishika ni jambo la kawaida kwenye maisha yetu ya kila siku.

Pale unapokutana na hali isiyo ya kawaida, pale unapopata ambacho hukutegemea, huwa unakuwa kwenye hali ya kutishika.

Lakini uzuri wa kutishika ni kitu cha muda mfupi, hutaendelea kutishika baada ya kitu kutokea.

Kilicho kibaya ni hofu, hofu huwa inaendelea hata baada ya tukio kupita, au wakati mwingine huwa inaanza hata kabla ya tukio husika. Hofu ni kitu endelevu, ambacho kinakuwa na madhara makubwa kwako.

Hofu inakuzuia usichukue hatua, inakupa wasiwasi, inakufanya usijiamini na hapo inakuwa kikwazo kwako kupiga hatua.

Huwezi kuzuia kutishika, kwa sababu ni kitu kinachotokea moja kwa moja pale hali usiyotegemea inatokea. Lakini unaweza kuzuia hofu isikutawale, kwa kujijengea ujasiri, kwa kuangalia kile unachoweza kufanya na kwa kuchukua hatua kwenye kile unachohofia.

Jiambie kabisa kwamba kujikuta kwenye hali ya mshangao au kutishika ni kawaida, lakini hutajiruhusu kuingia kwenye hofu, maana ukishakuwa na hofu, madhara huwa ni makubwa zaidi.

Na pia kumbuka, kutishika huwa kunakuja kama tahadhari kwako, lakini hofu huwa inakuja kuyafanya mambo kuwa mabaya zaidi ya yalivyo sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha