Ni nadra sana kila kitu kwenda kama unavyotaka kiende.
Hivyo kuacha kuchukua hatua mpaka wakati uwe sawa, kama unavyotaka wewe, ni kujichelewesha.
Katika kila wakati kuna kitu hakitakuwa sawa, kuna changamoto binafsi utakuwa nazo, kuna changamoto za kimazingira au kiuchumi zinaweza kuibuka.
Ukitaka sababu ya kutokufanya kitu chochote kile, utaipata haraka sana kwenye wakati kutokuwa tayari au kama unavyotaka.
Ukitaka sababu ya kufanya chochote utaipata ndani yako, pale unapokuwa umejitoa kweli kufanya na hukubali chochote kikuzuie.
Kwa kile ambacho umekuwa unapanga muda mrefu kufanya lakini wakati sahihi haupatikani,
Ninayo furaha kukujulisha kwamba wakati sahihi ni huu, hautapata tena wakati mwingine kama huu.
Siku unayoipata leo na kila siku ndiyo siku muhimu kwako kuitumia,
Acha kupanga na kupangua, badala yake anza kufanya.
Anza kwa hatua ndogo na endelea kuongeza mwisho utafikia hatua kubwa.
Anza kufanya kwa ukawaida na weka umakini usio wa kawaida na matokeo utakayoyapata yatakuwa siyo ya kawaida.
Siyo lazima uendelee na kile ulichoanza, kadiri unavyokwenda na kujifunza na kuona njia bora zaidi ya kufanya, chukua hiyo.
Unapojikuta njia panda, chagua kufanya kilicho sahihi, ambacho miaka kumi ijayo hutajutia kuwa umekifanya.
Usiangalie kuwaridhisha wengine, kila mtu anapambana na hali yake kama unavyopambana wewe. Kuhangaika nao ni kujichelewesha.
Kama mambo ni magumu kwako jua na kwa wengine ni magumu pia. Hata wale unaoona wanafanya vizuri, siyo kwamba mambo ni rahisi kwao.
Usisubiri shujaa yeyote kuja kukuokoa, hakuna anayekuja, hayo ni mapambano yako. Wewe pekee ndiye shujaa utakayejiokoa, ukishacha kusubiria shujaa mwingine aje.
Hata wale wanaosikitika na wewe, wanaokutia moyo na kukupa maneno mzuri, hakuna wanachoweza kukifanya zaidi ya maneno hayo. Mwisho wa siku maneno hayo hayatakutoa ulipokwama, au kukufikisha unakotaka kwenda. Ni lazima uamke na upambane.
Na hakuna wabaya kama wale wanaotaka kukusaidia kubeba matatizo yako, kupambana vita yako. Hata kama ni ndugu wa karibu au wazazi ambao wana uwezo fulani wa kukutoa pale ulipo, kufanya hivyo hakutakusaidia.
Kwa sababu baada ya kuvuka hapo siyo kwamba vita vimeisha, kuna mapambano mengine makubwa yanakusubiri, je hayo pia watakusaidia.
Usikubali misaada ya wale wanaotaka kupambana kwa niaba yako, wewe ulale tu na matokeo yaje. Hilo halitakujenga, litakufanya uwe tegemezi na kuna siku hawatakuwepo na hapo utaanguka vibaya.
Tangaza vita kila unapoianza siku yako, tangaza vita na uzembe, mazoea, uvivu na chochote kinachosimama kati yako na kile unachotaka. Na jiambie hiyo ndiyo siku ya ushindi, siku ambayo utapambana kweli kweli.
Huna nguvu ya kuchagua siku ijeje, huna nguvu ya kupanga mambo yaweje, lakini una nguvu ya kukabiliana na siku na yale yanayokuja kwenye siku hiyo. Kwa kuikabili kila siku yako kwa mtazamo huu, utakuwa na siku za ushindi ambazo zitatengeneza maisha ya ushindi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kwa somo zuri,kweli ukweli inabaki pale pale, Mimi tu ndio shujaa wa maisha yangu,hakuna wa kinipigania au kunipambania, naendelea kupambana kocha wangu,
LikeLike
Vizuri Beatus
LikeLike
Asante Coach kwa tafakari nzuri sana, Hakika jukumu la kupambana na changamoto zote za maisha linabaki kuwa mtu binafsi ,
Asante.
LikeLike
Karibu Joseph
LikeLike