Kwa asili sisi binadamu ni wabinafsi, huwa tunajali mambo yetu zaidi kuliko mambo ya wengine.

Na hakuna ubaya wowote kwenye hili, japo jamii inapenda kutuonesha kwamba ubinafsi ni mbaya, ukitumika vizuri ndiyo njia ya uhakika ya kufanikiwa.

Lazima uanze kwa kukiri kwamba chochote kile unachofanya ni kwa sababu yako binafsi. Unafanya kwa sababu ni kitu sahihi kwako kufanya, kwa sababu ndiyo kitu unachotaka kufanya.

Hufanyi ili uonekane, hufanyi ili usifiwe wala hufanyi ili ushinde. Badala yake unafanya kwa sababu umechagua kufanya.

Sasa hilo lina manufaa gani?

Kwanza unafanya kwa viwango unavyochagua wewe mwenyewe, kwa sababu hushindani na wengine wala hujaribu kuwaridhisha wengine.

Pili utafanya kwa usahihi, unapolazimishwa kufanya kitu unakifanya kwa namna isiyo sahihi. Ukichagua kufanya kitu wewe mwenyewe, unakifanya kwa usahihi, kwa sababu hujalazimishwa kukifanya, kama hutaki unaacha.

Tatu unakifanya kwa uhalisia, unaweka maisha yako kwenye hicho unachofanya na kwa namna hiyo utajitofautisha kabisa na wengine wanaofanya kitu kama hicho. Hilo linakufanya uwe tofauti na watu waje kwako kwa sababu unafanya kwa utofauti.

Hata kama unamsaidia mtu, humsaidii kwa sababu anataka msaada, bali unamsaidia kwa sababu umesukumwa kutoka ndani yako kufanya hivyo. Kwa sababu unataka kujisikia vizuri pale msaada wako unapokuwa na manufaa kwa wengine. Na pia unataka kusikia mwingine akikushukuru kwa msaada uliompa.

Chagua kuyaishi maisha yako na usiweke unafiki katika kuficha ubinafsi wako, badala yake utumie kwa manufaa, kuanzia kwako na kwa wengine pia.

Ukiwa na misingi sahihi unayoiishi, ubinafsi wako utakuwa na manufaa makubwa kwako na kwa wengine pia. Hivyo usiogope wala kujificha, jiweke wazi na ishi maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha