Tunaweza kufurahia kwamba enzi za utumwa zimepita na sasa kila mtu yuko huru.

Kwamba kile kipindi cha watu kuuzwa na kununuliwa kisha kumilikiwa na watu kama mali binafsi kimepita.

Kwamba zile zama za watu kufanyishwa kazi kwa shuruti na bila malipo hazipo tena.

Ukweli ni kwamba, utumwa haujaisha, utumwa bado upo na huu wa sasa una nguvu kuliko ule wa zamani.

Utumwa wa zamani ulikuwa wazi, mtu anaununiliwa na kumilikiwa. Utumwa wa sasa umejificha, mtu anajiuza mwenyewe bila kujua na kumilikiwa bila kujua.

Utumwa ninaouzungumzia hapa ni wa mitandao ya kijamii.

Makampuni yanayoendesha mitandao ya kijamii ni moja ya makampuni yenye mafanikio makubwa sana, yanaingiza fedha nyingi.

Umewahi kujiuliza fedha hizo zinatoka wapi? Maana hayana bidhaa zozote yanauza na wewe huduma zao unazitumia bure kabisa.

Usichojua ni kwamba, makampuni hayo yanakuuza wewe mtumiaji, yanauza taarifa zako kwa makampuni mengine yanayotaka kutangaza bidhaa zake.

Sasa unaweza kusema hakuna tatizo, hata wakiuza taarifa zako kwa watu wanaotangaza, kama kitu hutaki hutanunua.

Na hapo utakuwa unajidanganya, kwani makampuni hayo yanauza taarifa zako za ndani kabisa, kiasi kwamba makampuni yanayotangaza bidhaa mbalimbali yanajua jinsi ya kukushawishi ununue hata kitu usichokitaka.

Makampuni ya mitandao ya kijamii yana taarifa zako nyingi mno, tunaweza kusema yanakujua kuliko hata unavyojijua wewe mwenyewe. Hivyo yanakutumia wewe kama bidhaa na kuuza umakini wako kwa wale wanaoweza kuutumia kujiingizia faida.

Hiyo ni sehemu ya kwanza ya utumwa, kuuzwa kwa wengine.

Sehemu ya pili ya utumwa kwenye mitandao ya kijamii ni kufanya kazi usiku na mchana bure, unatumikishwa bila kulipa.

Hivi unafikiri unavyokazana kupata picha za kuposti kwenye mitandao hiyo, unavyokazana kupata wafuasi wengi, unavyojibu na kubishana na wengine kwenye mitandao hiyo, nani ananufaika? Mtandao husika ndiyo unaonufaika, kadiri unavyoutumia, ndivyo unavyokuwa na thamani zaidi.

Sasa swali ni je, masaa yote hayo ambayo umekuwa unaweka kwenye mtandao husika, unausaidia kukua, umelipwa nini? Sifuri, hakuna ulicholipwa, umetumikishwa bure, nguvu na muda mwingi umepotezea kwenye mitandao hiyo.

Rafiki, jua kitu kimoja, mtu pekee anayeweza kukutoa wewe kwenye utumwa ni wewe mwenyewe, kwa kuchagua kuishi maisha huru kabisa. Hakuna mwingine anayeweza kufanya hilo.

Tambua kwamba utumwa bado upo na utaendelea kuwepo kwa sababu watu hawajui jinsi ya kuwa huru. Na utumwa wa sasa ni mbaya kwa sababu umejificha, ila madhara yake ni makubwa.

Uhuru kamili ni kuondokana na utegemezi wa aina yoyote ile, kuchagua kile unachotaka na aina ya maisha unayotaka kuyaishi kisha kuishi maisha hayo. Kuepuka maisha ya maonesho au kuwaridhisha wengine na kutokujali wengine wanakuchukuliaje.

Kuwa huru na utayafurahia maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha