Ukweli huwa ni mgumu kuukabili,

Na pale ukweli unapokuwa mchungu, huwa tunatafuta uongo wa kutufariji.

Pale ambapo hatuna jibu sahihi kwa swali gumu, tunatengeneza swali jingine rahisi kwetu na kulijibu.

Hiyo ndiyo saikolojia ya mwanadamu, ndivyo ulivyo, japo hujawahi kujua hilo.

Wewe umekuwa unajiona una majibu ya kila kitu, kumbe sehemu kubwa ya majibu hayo ni maswali uliyoyabadili wewe mwenyewe.

Sasa tuje kwenye fursa mbalimbali ambazo watu wamekuwa wanaziona na kuzifanyia kazi.

Umesikia biashara A ni fursa nzuri, ukaingia kweli kuifanya. Umeanza kuifanya na hata bado hujavuna matunda ya fursa hiyo, unasikia tena biashara B ni fursa kuliko A.

Unajiambia hukubali kupitwa na fursa hiyo B, hivyo unajitosa pia kwenye biashara hiyo nyingine. Mambo yanaenda hivyo, kila wakati ni fursa mpya zinakuja kwako, huku zile za awali bado hujavuna matunda yake.

Kwa jinsi ambavyo hatupo tayari kuukabili ukweli, na kwa tabia yetu ya kutengeneza maswali rahisi pale tunapokabiliana na maswali magumu, fursa imekuwa moja ya vitu hivyo.

Kabla sijakufafanulia wacha nikuulize swali hili; unafanya biashara A, ambayo inakupa faida kubwa sana, ila pia ina wateja wengi na inataka muda wote wa biashara uwe hapo kwenye biashara na usiondoke hata dakika moja. Ukiondoka tu ni hasara. Biashara ina mafanikio makubwa kweli, lakini ni lazima uwepo muda wote. Swali ni je utakuwa tayari kutengeneza hasara kwenye biashara A ili uende kufanyia kazi fursa mpya ya biashara B? Hakuna anayeweza kufanya hivyo.

Kwa majibu ya mfano huo hapo juu, inakuwa wazi kwamba fursa mpya unazoziona siyo fursa kweli, bali ni njia ya wewe kutaka kutoroka kile unachofanya sasa. Kwa sababu labda ni kigumu kwako kufanya, au umekutana na changamoto au hakikulipi kama ulivyotarajia.

Lakini haupo tayari kuukabili ukweli kwamba kitu hicho ni kigumu au kimekushinda, hivyo unachofanya ni kutengeneza sababu ya kukuridhisha, kwamba umepata fursa nyingine nzuri kuliko hiyo ya awali.

Umefika wakati sasa wa kuacha kujidanganya na kuukabili ukweli kama ulivyo.

Na inapokuja kwenye shughuli unazofanya, hasa biashara, acha kuhangaika na kila fursa. Chagua biashara moja na weka juhudi zako zote mpaka upate matokeo mazuri. Usianze kuhangaika na mengine wakati bado hujafanya vizuri kwenye kile unachofanya sasa.

Stempu ya barua huwa inang’ang’ana kwenye bahasha moja mpaka ifike,

Unapowinda kundi la ndege unamlenga ndege mmoja na siyo kundi.

Na kwenye michezo ya mpira, wachezaji wengi wanakimbiza mpira mmoja.

Yote hayo yanatambua kanuni ya asili, kwamba kinachofanya vizuri ni kile kinacholenga eneo moja.

Watu wamekuwa wanasema waliofanikiwa wanafanya viti vingi, ni kweli kabisa, lakini wakati wanaanza hawakuanza na vitu vingi, walianza na vichache, wakaweka nguvu na vikafanikiwa, kisha wakaenda kwenye vitu vingine. Kama bado hujafanikiwa, usiangalie kile waliofanikiwa wanakifanya sasa, balia angalia kile walichokuwa wanafanya kabla ya kufanikiwa.

Fanya kitu kimoja na kifanye vizuri mno, kifanye kwa namna ambayo hakuna mtu mwingine amewahi kukifanya. Na wale unaowalenga wataona tofauti yako, na watakuwa tayari kushirikiana na wewe.

Kifanye kile ulichochagua kuwa ndiyo maisha yako, kuweka kila ulichonacho kwenye kukifanya kitu hicho, kujitoa kweli kweli na kila juhudi unayoweka italipwa mara dufu. Hizo juhudi ambazo ungeziweka kwenye vitu vingine, ziondoe huko na weka kwenye kile unachofanya sasa.

Swali utakalokuwa unajiuliza ni vipi kama nimegundua nilichochagua kufanya siyo sahihi? Ina maana siruhusiwi kubadilisha? Jibu liko wazi, unaruhusiwa kubadilisha sana, lakini usijidanganye. Kwamba ndani ya mwaka mmoja umejaribu fursa mpya tatu, na zote siyo sahihi kwako ila sasa umeiona ya nne ambayo ni sahihi? Hapo unajidanganya.

Angalia kwanza ni juhudi kiasi gani umeweka kwenye kitu, angalia ni ugumu kiasi gani unakabiliana nao na pia angalia wengine ambao wamewahi kufanya kitu hicho au kinafanana na hicho. Kama hujaweka juhudi za kutosha, huwezi kusema siyo sahihi kwako, ni uzembe wako tu. Kama unakabiliana na ugumu, una uhakika siyo unataka kuukimbia? Na kama kuna wengine wameweza kunufaika, kwa nini isiwe sahihi kwako, na hata kama hakuna, huenda wewe ndiyo wa kwanza.

Mzizi wa fitina ni kuwa mkweli na kuukabili ukweli bila ya kutafuta kujiridhisha au kutafuta swali rahisi kujibu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha