Ukiwa mkubwa unataka kuwa nani?
Hili ni swali ambalo kila mtu amewahi kuulizwa au kujiuliza kwenye hatua fulani ya maisha yake. Iwe ni wakati mtu yuko kwenye umri mdogo au nafasi ndogo, huwa anakuwa na picha fulani ya mtu atakayekuwa pale atakapokuwa na umri mkubwa au kupata nafasi kubwa zaidi.
Ukweli ni kwamba, swali hili linapotosha na limewapoteza walio wengi. Na hicho ndiyo jamii inataka.
Katika kujibu swali hili, mtu anaacha kuangalia ndani yake na kuanza kuangalia nje. Anaacha kujiuliza anataka nini na kuangalia wengine wanataka nini. Anaacha kujiuliza kipi chenye maana kwake na kuhangaika na kile ambacho wengine wanafikiri ndiyo chenye maana.
Katika kuhangaika na hayo, mtu anajisahau au kutokujijua na kuhangaika kuwa kama watu wengine. Ubaya ni kwamba, wale ambao mtu anahangaika kuwa kama wao, nao pia wanakazana kuwa kama wengine. Hivyo kinachotokea ni jamii ambayo inakazana kuwa kitu ambacho haikijui.
Njia pekee ya kuondoka kwenye mbio hizo zisizo na manufaa, njia pekee ya kuwa na maisha bora kwako, ni kuacha kutafuta utakuwa kama nani, na badala yake kuchagua kuwa wewe.
Ukiwa mkubwa au ukifika nafasi ya juu zaidi, kazana kuwa wewe zaidi. Fanya kile kinachotoka ndani yako, kile chenye maana kwako na kinachokupa hali ya kuridhika.
Najua una picha ya tofauti ndani yako, picha ambayo umewahi kuwashirikisha watu na wakakuambia hizo ni ndoto za kitoto, acha kujidanganya, kubali tu kile unachopata sasa. Ukawasikiliza na sasa unaendesha maisha ambayo huyafurahii. Ni wakati wa wewe kuifufua picha hiyo na kuanza kuiishi, bila ya kujali wengine wanachukuliaje au kama wanakubaliana nayo.
Unachohitaji wewe ni kuishi maisha yako, kitu ambacho jamii haipendi ukifikie, maana ukiweza kuishi maisha yako, utakuwa huru, hutaihitaji jamii na hapo jamii haiwezi kukushikilia mateka kama sasa na kukutumia itakavyo.
Jijue wewe mwenyewe kiundani na ishi wewe, pata muda wa kujitafakari na kuyajua maisha yako kiundani, kulijua kusudi lako na kisha kuchagua kuliishi. Haimaanishi kwamba maisha yatakuwa rahisi ukishajua kusudi lako na kuliishi, bali mapambano utakayoyakabili hayatakuumiza, utakuwa tayari kukabiliana na chochote kile.
Jamii haitaki ujue nguvu hii kubwa uliyonayo, ili uendelee kuwa kwenye kifungo. Mimi nimekuwa nakupigia kelele kuhusu nguvu hiyo kubwa uliyonayo, ili kwa namna yoyote ile, usinase kwenye mtego wa jamii.
Kuwa wewe, dunia inakuhitaji wewe kama wewe, ili uweke mchango wa kipekee kwenye dunia hii. Achana na jamii, achana na kundi kubwa na kuwa tayari kusimama mwenyewe, maana hakuna anayekujua wewe zaidi yako mwenyewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha,hili nililijua tu baada ya kujiunga kwenye kisima cha Maarifa, hakika huku ndio sehemu ya kujifunza, kujitambua kujielewa na kuweza kufanya uthubutu.asante Sana binafs nitaendelea kuweka juhudi kubwa kuhakikisha nakuwa Mimi wa ubora na hili nimeanza kulithibitisha kwa kuacha a na kufanya vitu vya mihemko, kufanya kitu kwa kuwa wengine wanafanya bali nafanya kama ni muhimu kwangu kufanya.
LikeLike
Vizuri sana Beatus kwa kujifunza na kuchukua hatua sahihi.
Kila la kheri.
LikeLike