Ukimchukua mtu yeyote aliyefanikiwa na kumfanya aanze upya safari yake ya mafanikio, ila arudie kila alichofanya kwa namna alivyofanya, hatafikia mafanikio aliyofikia.

Maamuzi ambayo mtu aliyafanya miaka iliyopita, akiyafanya tena leo hayatampa matokeo kama ya kipindi hicho.

Mazingira na hali ambazo mtu alikuwa anakabiliana nazo kwa kipindi kilichopita, siyo sawa na mazingira na hali atakazokabiliana nazo sasa.

Kila maamuzi ambayo mtu anayafanya ni mapya, hivyo kurudia kile kilichofanya kazi kipindi cha nyuma haitaleta matokeo sahihi.

Kuna funzo kubwa sana la kujifunza hapa, kutokukariri maisha, kutokuishi kwa mazoea. Haijalishi nini kimefanya kazi jana, leo unakabiliana na hali tofauti, inakutaka ufanye maamuzi ambayo ni tofauti.

Hapo utajiuliza ya nini kujifunza sasa, kama ya nyuma hayana msaada kwenye kufanya maamuzi sasa.

Jibu ni kujifunza ni muhimu mno, kwa sababu kunakujengea uwezo wa kufanya maamuzi ambayo ni sahihi.

Kwa kukumbuka maamuzi uliyofanya nyuma na matokeo uliyopata, kwa kukumbuka maamuzi waliyofanya wengine ambao umejifunza kwako na kisha kutathmini kile unachokabiliana nacho, akili yako itaweza kuchakata na kuja na maamuzi ambayo ni bora zaidi.

Kumbuka kila unachofanya kwenye maisha yako kinajenga kumbukumbu kwenye akili yako, na pale mazingira na hali zinapojirudia, akili inakumbuka hatua zipi ulizochukua.

Mara nyingi akili yako itakuwa inakupa majibu ya haraka, lakini hayo huwa siyo sahihi. Unapaswa kuzuia majibu hayo na kutathmini kwanza kile unachokabiliana nacho, kuangalia kila kinachohusika nacho na kisha kufanya maamuzi sahihi.

Kumbuka kila maamuzi unayofanya ni maamuzi mapya, hivyo yape uzito, yatathmini kwa kina na fikia maamuzi sahihi.

Na kwa kila maamuzi unayoyafanya, tafakari matokeo unayopata na ondoka na somo ambalo litakuwezesha kufanya maamuzi bora zaidi baadaye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha