Fikiria unafanya kazi ambayo inahitaji umakini wako, ghafla unaingia ujumbe kwenye simu yako. Unajiambia utauangalia na kuujibu kisha kurudi kwenye kazi yako, itakuchukua dakika moja tu.

Hapo jua wazi kwamba unajidanganya, siyo dakika moja utakayotumia kuangalia na kujibu ujumbe kisha kurudi kwenye kazi, itakuchukua muda mrefu zaidi ya hapo.

Kitendo cha kuuangalia ujumbe, kuusoma na kuuelewa, kisha kufikiria namna gani ya kuujibu kwa usahihi, itakuchukua muda.

Na hata kama utajibu kweli ndani ya dakika moja, bado utaendelea kufikiria kuhusu ujumbe huo kwa muda. Utafikiria atakujibuje mtu huyo. Akichelewa kujibu utajiuliza ameuelewaje ujumbe huo, au umemjibu isivyo sahihi, au umemkwaza, hayo ni maswali utakayokuwa unajiuliza.

Hilo litakugharimu muda mwingi kuliko dakika moja uliyojiambia itakuchukua.

Hata kama hutafikiria ujumbe huo, kitendo cha kukatisha kazi na kupeleka umakini wako kwenye kitu kingine, kinakurudisha nyuma kidogo. Hutaweza kurudi na kuendelea pale ulipoishia kwa kasi ile ile, badala yake utarudi nyuma na kasi yako itakuwa chini.

Kila unachofanya, kinakugharimu muda mwingi kuliko unavyofikiri. Kitendo cha kuingia mitandaoni, kinagharimu muda mwingi. Hata kuweka tu picha kwenye mitandao ya kijamii, itakuchukua muda kufikiria picha ipi sahihi, watu wataichukuliaje na mengine mengi.

Ukishaiweka kila mara utatazama wangapi wameipenda na maoni gani wengine wameyatoa. Kama imependwa na wachache unaanza kujisikia vibaya, labda siyo picha nzuri, labda watu hawakujali. Ikitokea mtu mmoja ameweka maono mabaya, ndiyo unavurugikiwa kabisa, unaona kama ameharibu maisha yako yote.

Kitu muhimu sana cha kujifunza hapa ni kimoja, njia unayotumia kupima muda siyo sahihi, kupima muda utakaokwenda kutumia ni kujidanganya, badala yake pima muda ambao tayari umeshautumia kwenye kitu.

Na muhimu zaidi, unapofanya kazi inayohitaji umakini wako mkubwa, weka umakini wako wote kwenye kazi hiyo, usiruhusu mawazo yako kwenda kwenye kitu kingine chochote.

Ni bora kuweka umakini wako kwenye kazi kwa muda mfupi kisha kuwa na muda wa kuruhusu usumbufu, kuliko kufanya kazi yako kwa muda mrefu huku ukiwa na usumbufu.

Kutenga saa moja ya kufanya kazi ambayo hutakuwa na usumbufu itakuwa na tija kuliko masaa matatu ya kufanya kazi huku ukiruhusu kila aina ya usumbufu.

Kumbuka muda ni rasilimali adimu, hakuna anayeweza kupata muda zaidi, hivyo wajanja kwenye muda ni wale wanaopunguza mambo ya kufanya, kuachana na yasiyo muhimu na kufanya yaliyo muhimu pekee.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha