Watu wamekuwa wanajipa majukumu ambayo siyo tu yako nje ya uwezo wao, bali pia yanawapoteza. Yanawapoteza kwa sababu nguvu wanazotumia kuhangaika na majukumu hayo, ni nguvu ambazo hawawezi kuzitumia kwenye yale muhimu kwao, hivyo zinapotea na hawapati matokeo yoyote mazuri.
Dhana kwamba unataka kuibadili dunia ni moja ya majukumu ambayo unajipa na yanakupoteza. Kutaka kila kitu kiende kama unavyotaka wewe, kila mtu awe kama unavyofikiri wewe ni kitu kisichowezekana kabisa. Lakini wengi wamekuwa wanajisumbua kwa hilo.
Hii ina maana kwamba ukubali kushindwa, uende tu kwa mazoea kwa sababu huwezi kuibadili dunia au kuwabadili wengine? Jibu ni hapana, kuna mengi unayoweza kufanya na ukapata matokeo mazuri.
Moja ya hayo ni kubadili jinsi unavyoiangalia dunia, hicho ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako na unaweza kukitumia kufanya makubwa.
Wale waliofanya uvumbuzi mkubwa unaoonekana kuibadili dunia, hawakuanza na lengo la kuibadili dunia, bali walianza kwa kuiangalia dunia kwa namna tofauti. Wakati wengine wakiipokea dunia kama ilivyo na kuishi kwa mazoea, wao waliiangalia dunia kwa utofauti na kisha kuweka kazi kufikia utofauti huo.
Hivyo chenye nguvu hapa ni maono, jinsi gani unaiona dunia ndivyo unavyopata nguvu ya kufanya makubwa au kukata tamaa na kuacha.
Kwanza kabisa jifunze kuona upande chanya wa kila jambo, hata kama kuna kitu kibaya kiasi gani kimetokea, kuna upande wake chanya, angalia huo na utaona jinsi ya kutumia kitu au hali hiyo kwa manufaa zaidi. Hii pia inaenda kwa watu, badala ya kuyaangalia madhaifu ya watu na kuona hawafai au unapaswa kuwabadili, angalia uimara wao na jinsi ya kushirikiana nao kwenye hilo. Hakuna mtu asiye na manufaa kabisa, inategemea unamwangaliaje.
Kingine kikubwa cha kubadili ni mtazamo ulionao, kuwa na mtazamo wa uwezekano na wa mambo makubwa wakati wote. Haijalishi kitu kipo chini kiasi gani, kione kikiwa kikubwa, hata kama kitu hakijawahi kufanyika, kione kikiwezekana kufanyika.
Jinsi unavyoiona dunia inakupa nguvu kubwa ya kufanya makubwa kwenye dunia hii. Hendry Ford aliiona dunia yenye watu wanaosafiri kwa magari, kisha kufanya kazi na kufikia dunia hiyo. Bill Gates aliiona dunia yenye watu wanaotumia kompyuta kwenye kazi zao za kila siku, akafanyia kazi na kufikia dunia hiyo. Elon Musk anaiona dunia ambayo watu wanaenda angani na kwenye sayari nyingine kwa matembezi au kubadili maisha, anafanyia kazi kufikia dunia hiyo.
Swali ni je wewe unaiona dunia ya aina gani? Tengeneza maono ya dunia unayoona inapaswa kuwa, kisha fanya kazi kufikia dunia hiyo. Hapa hujaribu kuibadili dunia, bali unaiikia dunia ambayo ipo, ila wengine hawajaweza kuifikia bado.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,