Moja ya madhara hasi ya mitandao ya kijamii, ni kufanya kila mtu afikiria kufikia watu wengi. Kwa kuwa mitandao hii inatupa nafasi ya kuwa na marafiki wasio na kikomo dunia nzima, hata soko letu nalo pia limebadilika. Tunasukumwa kumfikia kila mtu, na hapo ndipo tunapoharibu.
Kwa chochote unachofanya, unapolenga kumfikia kila mtu, unaishia kutokumfikia yeyote, kwa sababu kundi kubwa la watu hawawezi kufanana kwa yale ya kipekee.
Inachotokea ni watu wanakimbizana na mchezo wa namba, kama tunavyoangalia wingi wa marafiki au wafuasi mitandaoni.
Badala ya wewe kuanguka kwenye mtego huo, unapaswa kuachana na kundi kubwa, achana na namba kubwa na anza na kikundi kidogo. Kwa chochote unachofanya, angalia kikundi kidogo cha watu wa tofauti unachoweza kuanza nacho, kisha anza na hicho.
Achana kabisa na kuangalia namba kubwa ya watu, bali wewe angalia kile kikundi ulichoanza nacho na hakikisha unakihudumia vizuri.
Kwa kufanya hivi, unagundua mambo mawili makubwa,
Kwanza kikundi hakitakuwa kidogo kama ulivyokuwa unachukulia awali, kwani utagundua kina mahitaji mengi kuliko ulivyokuwa unategemea, hivyo utaweza kuzama zaidi na kukinufaisha huku wewe ukinufaika pia.
Pili kikundi kitakua bila ya wewe kuhangaika sana, maana hao unaowahudumia nao watawaleta wengine wanaofanana nao. Hivyo kazi yako inajitangaza yenyewe na kuwavutia wengine kuja kwako.
Anza na kikundi kidogo na peleka nguvu zako zote katika kuhudumia kikundi hicho, na utashangaa jinsi utakavyoweza kufanya makubwa kwa kuanza na kikundi hicho kidogo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,