Mtu mmoja amewahi kusema kwamba kitu pekee tunachojifunza kwenye historia ni kwamba hatujifunzi kupitia historia.

Ukiangalia hapa duniani, mambo ni yale yale, yamekuwa yanakuja kwa njia tofauti. Hivyo kama tungekuwa tunajifunza kupitia historia, tungeepuka kurudia makosa yanayotugharimu.

Lakini hatujifunzi kupitia historia, ndiyo maana tunarudia makosa yale yale na yanatugharimu sana.

Na hii ni kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, jamii, taifa na dunia kwa ujumla. Historia ina mengi ya kutufunza, lakini hatuna muda wa kujifunza, hivyo tunarudia makosa yale yale.

Kila ukiangalia maisha ya watangulizi wetu, kuna mambo ambayo ukiyaona unacheka, unajiambia kweli hawa watu walikuwa wanaamini hivyo.

Fikiria imani potofu nyingi ambazo watangulizi wetu walikuwa nazo, kuhusu watoto, wanawake, watu wenye ulemavu, dini, ushirikina na mengine. Leo ukiangalia kile walichokuwa wanaamini, unacheka na kushangaa.

Lakini kwa kipindi chao ilikuwa ni vitu vikubwa, vitu ambavyo watu walivipa uzito, walibishana, waliingia kwenye mapigano ili kuvitetea. Lakini leo hii, tunaona ni ujinga.

Angalia vita za kidini au kikabila, hata vita za taifa kwa taifa na mpaka vita kuu za dunia ambazo zimewahi kuwepo. Leo ukichunguza nini kilipelekea mapigano hayo, unakuta ni vitu vidogo vidogo ambavyo leo ukiviangalia unacheka, kwamba kweli dunia nzima iliamini ni sahihi watu kuuawa kwa sababu hizo?

Kitu kikubwa cha kujifunza hapa na kujifunza kwenye historia ni kwamba, jambo lolote lile, baada ya muda huwa linaonekana ni la kijinga. Japo kwa wakati wake jambo hilo linaweza kuwa na umuhimu na kuaminiwa na wengi, lakini baada ya muda vinapoteza umuhimu wake.

Hiyo ni kusema kwamba, kwa kila unachohangaika nacho leo, siku zijazo watu watakiangalia na kucheka, hawataamini kwamba kuna watu walikuwa makini kabisa kuamini kitu kama hicho.

Hoji kila kitu, usipoteze muda wako kuhangaika na mambo ambayo yanapita, kujisumbua na yasiyodumu. Siyo lazima uwe na maoni kwenye kila jambo na pia jipe muda kwenye kila jambo, usisumbuke na yasiyokuwa na tija kwako.

Pia jifunze kupitia historia, angalia makosa ambayo wengine walifanya kipindi cha nyuma na hakikisha hurudii kufanya makosa hayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha