Kuna biashara au kazi ambazo mtu unaweza kufanya kwa muda mfupi, ndani ya mwaka mmoja na kuachana nayo kwenda kwenye biashara nyingine. Biashara za aina hiyo huwa hazihitaji vigezo vingi, hapo unaangalia tu faida unayokwenda kupata.
Halafu kuna biashara au kazi ambazo mtu unataka kufanya kwa muda mrefu, unapanga kufanya kitu hicho kwa miaka yako yote, hapo unaongelea miaka 30 mpaka 50 ya kufanya kitu hicho. Kwa hii, unahitaji kuwa na vigezo sahihi vya kuzingatia ili baadaye isiwe kikwazo kwako.
Hebu fikiria umechagua biashara au kazi ambayo unataka ufanye maisha yako yote, lakini miaka 10 baada ya kuwa kwenye biashara au kazi hiyo inakuwa haina thamani tena. Hivyo miaka 10 uliyoweka umeipoteza na inabidi uende kuanza eneo jingine upya kabisa.
Kuondokana na hilo, leo tunakwenda kujifunza vigezo vitano vya kuzingatia, kwa kuzingatia vigezo hivi, utaweza kufanya maamuzi sahihi na hata kuendelea kuboresha maamuzi yako ili ufanye kitu cha uhakika.
Kabla hatujaangalia vigezo hivyo, tuanze na mfano huu. Umehamia eneo ambalo hakuna duka karibu, unaona kuna fursa ya kufungua duka. Unalifungua na kutengeneza faida nzuri, biashara ni rahisi na haikusumbui, mambo yanakwenda vizuri. Baada ya muda, watu wanaona hiyo ni fursa pia, nao pia wanafungua biashara hiyo ya duka. Baada ya muda mtaa unakuwa na maduka mengi na mnagawana wateja, kitu ambacho kinakuwa kikwazo kwa ukuaji wako.
Vigezo vitano vya kuzingatia.
Karibu kwenye vigezo hivi vitano vya kuzingatia ili ujenge kazi au biashara yenye manufaa kwako kwa muda mrefu.
Kigezo ha kwanza ni ugumu wa kujifunza na kufanya.
Watu wanapenda vitu rahisi, hivyo kama kazi au biashara unayofanya au kutaka kufanya ni rahisi kujifunza na kuifanya, basi jua wengi wataifanya na hilo litashusha thamani yake. Ni kanuni ya uchumi kwamba kadiri kitu kinavyopatikana kwa urahisi, ndivyo thamani yake inavyokuwa chini.
Chagua kufanya kazi au biashara ambayo ni ngumu kujifunza na ngumu pia kufanya. Ugumu huo unawazuia wengi wasiingie na hivyo wachache mnaoifanya mnathaminiwa na hivyo kunufaika nayo.
Kigezo cha pili ni kipaji maalumu kinachohitajika.
Hii pia inaendana na hapo juu, unapaswa kufanya kazi au biashara ambayo inahitaji kipaji maalumu kwa anayeifanya, na wewe uwe na kipaji hicho. Wale wasio na kipaji wanakwamishwa kuingia hivyo thamani inakuwa juu.
Kigezo cha tatu ni kuwahi na nafasi ya kutawala soko.
Ukishasikia fursa inazungumziwa na kila mtu, basi jua umeshachelewa. Fursa nzuri ni ile ambayo unaipata mapema kabla kila mtu hajaijua, kisha unatawala sehemu ya soko hilo hivyo inapokuwa maarufu na wengi kuikimbilia, wanakukuta wewe umeshatawala soko hilo.
Kigezo cha nne ni kitu cha kipekee kinachokutofautisha.
Unapaswa kuwa na kitu cha kipekee kinachokutofautisha na wengine wanaofanya kazi au biashara kama yako. Inaweza kuwa na taarifa fulani ulizonazo wewe na wengine hawana, au kuna wazo ambalo umelifanyia hatimiliki na hivyo ni lako tu, hakuna mwingine anayeweza kulitumia. Pia inaweza kuwa ni namna unavyoweka utu wako kwenye kazi au biashara yako.
Kama usipokuwepo watu hawaoni pengo lako, upo eneo ambalo siyo sahihi. Pengo lako linapaswa kuonekana na asiwepo wa kuliziba.
Kigezo cha tano ni fursa ya kukua zaidi kadiri unavyokwenda.
Kitu unachofanya kwa maisha yako yote, lazima kiwe na fursa na nafasi ya kukua zaidi. Kufanya kitu kwa namna ile ile huku ukibaki kwenye kiwango kile kile siyo tu inakuweka kwenye hatari ya kuzidiwa na wengine, lakini pia inakupa uchoshi wewe mwenyewe.
Hivyo ingia kwenye kazi au biashara ambayo kadiri miaka inavyokwenda unajijengea uzoefu na ubobezi mkubwa. Unavyozidi kuwa kwenye tasnia hivyo, ndivyo thamani yako inavyozidi kukua na hivyo kunufaika zaidi.
Zingatia hayo matano kama bado hujafanya maamuzi, na kama umeshachagua kazi au biashara utakayofanya maisha yako yote, basi tengeneza vigezo hivyo vitano pale ulipo sasa na utaweza kupiga hatua kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante sana.
LikeLike