Kama umewahi kutumia ramani kufika mahali au kukamilisha jambo, unajua wazi kabisa uhalisia huwa hauendi kama ramani kwa asilimia 100.

Hata kama ni ramani ya nyumba umechorewa vizuri, ukaipenda kweli kweli na ukawa na kiasi cha fedha cha kutosha kutekeleza kila kilichopo kwenye ramani, bado nyumba iliyokamilika haitafanana na ramani kwa asilimia 100.

Mara zote, uhalisia huwa unatofautiana na ramani, hata kama ni kwa kiwango kidogo. Hata kama utaifuata ramani kama ilivyo bila ya kubadili chochote.

Kwa kujua hili kunatupa uhuru mkubwa kwenye mipango mbalimbali ambayo tunaiweka.

Kabla hujaanza kitu chochote, huwa unajiwekea mipango, lakini mipango hii ni makadirio, ni kama ramani, inaonesha nini unataka na utakipataje.

Utakapoingia kwenye ufanyaji, siyo kila kitu kitaenda kama mipango uliyoweka. Kutakuwa na mabadiliko, kutakuwa na vitu ambavyo hukuvitegemea.

Hivyo pamoja na kuwa na mipango, haimaanishi huo ndiyo msahafu, badala yake unapaswa kupima kila unalokabiliana nalo na kisha kuboresha zaidi mpango ulionao.

Wakati unaweka mipango hukuwa na uhalisia, hivyo unapofika kwenye uhalisia na kujifunza yale ambayo hukuyajua wakati unaweka mpango, unapaswa kuboresha mpango wako ili uweze kuendana na uhalisia.

Kuweka mipango ambayo inakwenda tofauti na uhalisia haimaanishi kwamba mipango hiyo imeshindwa, bali ni fursa kwako kuboresha mipango yako. Muhimu ni kujua nini hasa unachotaka na kwa kila maboresho unayofanya, yakufikishe kwenye kile unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha