Ukitapa kufikia ubobezi na mafanikio kwenye eneo lolote la maisha yako, unapaswa kuweka juhudi zako kwenye vitu vidogo vidogo, ambavyo ndiyo msingi mkuu wa eneo hilo.

Na siyo tu kuvijua, maana tayari unavijua, bali kuvifanya.

Angalia eneo la fedha, msingi mkuu uko kwenye kupunguza matumizi, kuongeza kipato na kuwekeza. Hakuna kingine zaidi ya hapo ambacho ni cha msingi.

Ukienda eneo la afya, msingi mkuu upo kwenye ulaji, mazoezi na kupumzika.

Kadhalika kwenye biashara, unahitaji kuwa na bidhaa au huduma, ambayo inatatua tatizo ambalo watu wanalo kisha kuwafikia watu hao na kuweza kuwashawishi kununua.

Misingi hii inaeleweka kwa urahisi na karibu kila mtu anaijua.

Tatizo liko kwenye kuiishi, kwa sababu unapaswa kuiishi kila siku, siyo kitu cha kufanya mara moja ukawa umemaliza, ni kitu unachopaswa kufanya kila siku.

Na hivyo ndivyo ubobezi unavyokuja, kwa kujua misingi hiyo na kuifanyia kazi kila wakati.

Kwa kuwa kurudia rudia vitu hivyo kunaleta uchoshi na kwa kuwa inahitaji muda mpaka mtu uanze kupata matokeo unayotaka, wengi wamekuwa wanadharau hatua hizo na kuanza kutafuta mambo magumu.

Huwa tunafikiri mafanikio makubwa yanatokana na kufanya mambo magumu na makubwa mara moja. Na hata wanaotaka kututapeli huwa wanakuja na gia hiyo. Wanakuonesha ipo njia ya mkato ya kufika unakotaka kufika mapema, lakini ni ngumu na huwezi kuielewa vizuri wewe mwenyewe, hivyo unawahitaji wao ili wakusaidie. Na hapo unaishia kuwanufaisha huku wewe ukibaki bila manufaa.

Kwenye kila eneo la maisha yako, ijue misingi na iishi.

Kwa kukumbushana, zingatia maeneo haya;

  1. Kwenye maisha kwa ujumla; NIDHAMU, UADILIFU, KUJITUMA.
  2. Kwenye kuweka vipaumbele vyako; AFYA. UTAJIRI, HEKIMA.
  3. Kwenye kazi; KAZI, UPENDO, HUDUMA.
  4. Kwenye fedha; KIPATO, AKIBA, UWEKEZAJI.
  5. Kwenye mahusiano; UPENDO, MUDA, KUJALI.
  6. Kwenye uongozi; MAONO, MASLAHI, KUJALI.
  7. Kwenye kujifunza; UBORA, TAFAKARI, HATUA.
  8. Kwenye uwekezaji; MAPEMA, MSIMAMO, MUDA.
  9. Kwenye biashara; THAMANI, MASOKO, MAUZO.
  10. Kwenye mafanikio; MAARIFA, HATUA, MAFANIKIO.

Hii ni misingi midogo midogo ambayo ukiweza kuiishi kila siku, utapiga hatua kubwa kwenye kila eneo la maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha