Hasira ni moja ya hisia ambazo huwezi kuzifuta kabisa kwenye maisha yako.
Hivyo wale wanaoonekana kama hawana hasira, siyo kwa sababu wamezifuta hasira, ila kwa sababu wamejua jinsi ya kuzidhibiti.
Na wale wanaoonekana kuwa na hasira sana, ni kwa sababu hawana udhibiti kwenye hisia zao.
Hasira ni hisia zinazoibuka kwa asili pale mambo yanapokwenda tofauti na tulivyotegemea, na hisia hizo huwa kali pale tunapojua kuna mtu mwingine amehusika katika hilo.
Hasira zinakusukuma uchukue hatua fulani ili uone kwamba hujapoteza, au hata kama umepoteza basi kuna namna umelipa. Kinachotokea ni madhara ya hasira hizo yanakuwa makubwa na yanayokusumbua zaidi baadaye.
Hivyo dawa ya hasira ni kuchukua hatua, lakini ambazo hazitamhusisha mtu mwingine, zikuhusishe wewe mwenyewe.
Mfano kama ni mtu amekukasirisha na unataka kumjibu kwa hasira ulizonazo, chukua kalamu na karatasi kisha andika kila unachotaka kumjibu, andika kwa hasira zako zote, usiache hata kitu kimoja. Kama unataka kumtukana mtukane kweli kweli, mweleze kila unachotaka, kisha hifadhi hicho ulichoandika mahali salama. Baada ya siku mbili au hasira ikiwa imeshatulia, rudi usome ulichoandika, utashangaa kweli kweli.
Zoezi hilo la kuandika linakupa wepesi kwa sababu unakuwa umetua mzigo mzito ulio ndani yako, na kutokutuma ulichoandika kunaondoka madhara ya kusumbuana zaidi. Baadaye unapokuja kusoma unajifunza jinsi hasira zilivyo mbaya. Na katika wakati huo, choma moto kile ulichoandika na utakuwa huru zaidi.
Kadhalika kama mtu amekuudhi na unataka kumpiga, hizo nguvu za kumpiga zitumie kufanya kitu kingine, labda fanya matembezi au fanya zoezi lolote lile. Lengo ni kuhakikisha nguvu hizo zilizochochewa na hasira unazitoa kwenye mwili wako, kwa namna ambayo huhusishi mtu mwingine. Baadaye ukiwa umeshatoa nguvu hizo na kutulia, utaweza kujua kipi sahihi cha kufanya.
Tunachojifunza hapa ni kwamba hasira huwa zinatujaza nguvu kubwa inayotusukuma kuchukua hatua. Hatua ambazo hasira inatusukuma kuchukua ni zenye madhara kwa wengine, hivyo tunachopaswa kufanya ni kugeuza hatua hizo, kwa kufanya kitu kingine kitakachotumia nguvu hizo, lakini hakihusishi mtu mwingine. Hilo litasaidia hasira ziishe haraka.
Hii ina manufaa kuliko kuzuia hasira hizo ndani yako, na kuiacha nguvu inayotengenezwa na hasira ikae ndani yako, lazima itakusukuma kufanya kitu kisicho sahihi. Hivyo kwa kujisukuma wewe kufanya kilicho sahihi, unatumia nguvu hizo na kuepuka madhara yake.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Nikiwa na hasira nakaa pekee yangu navuta pumzi ndani nakutoa nje mara 10 baada ya hapo hasira zote zinaisha, sababu usipo dhibiti hasira unaweza kufanya jambo jamii ikawa inakudharau ,tangia nijuwe njia hiyo nimekuwa bora sana
LikeLike
Vizuri Mary kwa zoezi hilo zuri ambalo umekuwa unafanya kukabiliana na hasira.
LikeLike
Ahsante sana kocha, nimekuwa natumia mbinu ya kukaa kimya. Nakwenda kuongeza mbinu hizo mbili ili kujiweka mbali na hasira.
LikeLike
Vizuri Tumaini, kila la kheri.
LikeLike